Warejeshewa hela zao baada ya corona kutatiza maonyesho
Na DIANA MUTHEU
MAMIA ya watu wamerejeshewa hela zao baada ya janga la corona kutatiza maonyesho ya kilimo ambayo yaliratibiwa kufanyika kuanzia mwezi wa Agosti hadi Septemba katika Kaunti ya Mombasa.
Akizungumza na Taifa Leo, mwenyekiti wa kamati ya maonyesho hayo, Bi Anisa Abdalla alisema kuwa baadhi ya watu walikuwa tayari wamejisajili kushiriki katika maonyesho hayo, lakini baada ya janga hilo kusambaratisha mipango yote, waliomba kurejeshewa fedha zao.
Alithibitisha kuwa shughuli hiyo ilifaa kuanza mnamo Agosti 26 hadi Septemba 1 mwaka huu, katika uwanja wa Mkomani, Nyali.
“Tuna matumaini kuwa hali itarejea kama kawaida. Iwapo itatubidi kuendelea kuishi na janga hili, basi nasi itatubidi tuje na teknolojia mpya ya kuhakikisha kuwa maonyesho yanafanyika,” akasema Bi Abdalla.
Kwa kawaida, maonyesho haya huwavutia zaidi ya watu 3,000 kila mwaka kutoka humu nchini na hata wageni kutoka nchi za nje.
Pia, mashirika mbali mbali ya hapa nchini kama vile Halmashauri ya Bandari Nchini (KPA), mabenki hupamba vibanda vyao na majengo ambayo hutumiwa kuonyesha bidhaa na huduma zao.
“Maonyesho ya kilimo ambayo yalifanyika mwaka huu ni yale ya Eldoret na Embu, na yalikuwa mwanzoni mwa mwaka huu kabla kisa cha kwanza cha mgonjwa aliyeambukizwa virusi vya corona kutangazwa nchini,” akasema.
Katika maonyesho haya, wanaohudhuria huweza kufundishwa mbinu mpya za ukulima na pia wakaweza kujionea mavumbuzi mapya.
Mkazi mmoja wa Mombasa ambaye pia ni mvumbuzi, Bw Abraham Gatene alisema kuwa maradhi ya Covid-19 yamewazuia baadhi ya wavumbuzi nafasi ya kukutana na wawekezaji.
“Maonyesho ya kilimo yamekuwa mahali pa vijana ambao wanatumia teknolojia kuimarisha kilimo kukutana na wawekezaji ili miradi yao ipigwe jeki, na kuna wengi ambao tayari wamefaidika. Hata hivyo, mwaka huu kwa sababu ya janga hili, itatubidi tutafute njia mbadala,” akasema.