Habari Mseto

Warsha ya kukabili uhalifu mijini yaandaliwa

September 15th, 2019 Kusoma ni dakika: 1

 NA RICHARD MAOSI

Shirika la kibinafsi linalosimamia haki za kibinadamu (Midrift Human Rights), kutoka Nakuru liliandaa warsha ya siku tatu kuwafundisha wakazi namna ya kukabiliana na uhalifu unaotendeka mijini.

Kampeni hiyo iliwaleta pamoja washikadau kutoka eneo la Naivasha na Nakuru, ili kuwapatia ujuzi wa kujiboresha kupitia miradi ya kujiinua kimaisha kama vile ujasiriamali.

Akizungumza na Taifa Leo Dijitali Dkt Robert Worrall kutoka Ireland, mtaalam wa maswala ya uongozi alisema hii ni njia moja ya kuwafanya vijana kuwa katika mstari wa mbele kuhubiri amani.

Tangu 2016 Robert amekuwa akishirikiana na viongozi kadhaa kutoka Nakuru, kwa kuleta idara mbalimbali pamoja,kujadili changamoto zinazowakumba vijana mitaani.

Viongozi 50 kutoka Nakuru na Naivasha walishirikishwa, 25 kutoka kila upande,baada ya kupenya mchujo uliowapatia fursa ya kupokea mafunzo hayo ya siku tatu yaliyoanza rasmi siku ya Jumatano na kukamilika siku ya Ijumaa mjini Nakuru.

“Tunashirikiana na viongozi hawa ili watusaidie kuumba upya dhana katika mawazo ya vijana kuwa maisha yanawezekana bila kutegemea uhalifu,” Robert alisema.

Baadhi ya wakazi kutoka Nakuru na Naivasha wakipokezwa vyeti na Robert Worrall (kushoto) baada ya kushiriki mafunzo namna ya kukabiliana na uhalifu mijini. Picha/Richard Maosi

Viongozi hao walijadiliana kwa kina na kuja na malengo ya muda mrefu yatakayowasaidia kuwafikia vijana wengi wenye azma ya kujinasua kutoka kwenye changamoto za mihadarati.

Kando na hayo waliratibu utaratibu wa kuendesha shughuli zao kwa kutoa udhamini kwa miradi midogomidogo mashinani ya kuwashirikisha vijana wawe watu wa kujitegemea.

Mno wakilenga Kenya na Uganda (Mbale) ambapo wanaungama kuwa vijana wanaweza kujifundisha kutokana na hali halisi ya maisha,ikiwemo umaskini na uhalifu.

Tume nyingine zinazolengwa kuhusishwa ni pamoja na Polisi,wahudumu wa afya,idara ya magereza na mashirika yanayotetea haki za kibinadamu.

Rob anasema hii itatoa nafasi ya viongozi kuhudumia jamii kwa namna ipasavyo,kitaaluma kwa kupata ufadhili kutoka mataifa ya nje.