Washukiwa wa 37 wa NYS walia wanasiasa kudai lazima watafungwa
Na RICHARD MUNGUTI
WASHUKIWA 37 katika kashfa ya Sh226 milioni iliyokumba shirika la huduma ya vijana kwa taifa akiwamo aliyekuwa katibu mkuu Lillian Omollo Jumatano waliomba mahakama iwazuilie wanasiasa wakuu nchini kukoma kuahidi mahakama itawafunga.
Mawakili wakiongozwa na Bw Assa Nyakundi waliteta kuwa baadhi ya wanasiasa wamekuwa wakifanya ziara ng’ambo na humu nchini wakitoa ahadi ambazo hawawezi kuzitimiza.
“Katika siku za hivi punde baadhi ya maafisa wakuu serikalini na wanasiasa wamekuwa wakiahidi washukiwa katika kesi hii ya kashfa ya NYS watafungwa bila shaka,” alisema Bw Nyakundi.
Wakili huyo alisema, “Ni wewe unasikiza hii kesi mbona wanasiasa wanazugumza kama ni wao watawafunga washukiwa hawa. Naomba hii mahakama iwazime kujadili na kuzugumzia kesi hii katika hafla za umma.”
Bw Nyakundi alimweleza Bw Ogoti kuwa yapasa wanasiasa na wakuu serikalini wakumbushwe kuwa kuna sheria inayowazuilia watu kujadilia kesi ikiendelea mahakamani.
Hakimu alielezwa kuwa ni yeye anayesikiza kesi na kamwe “ wanasiasa hawapasi kukubaliwa kuendelea na kujadilia kesi hii adharani na midahalo ya kimataifa.”
Rais Uhuru Kenyatta amekuwa akisema katika hafla mbali mbali kwamba idara ya mahakama itawafunga washukiwa wanaodaiwa waliiba mamilioni ya pesa kutoka NYS.
Wakili Migos Ogamba alisema sheria yapasa kutumiwa kuwalinda washukiwa dhidi ya shutuma kutoka kwa umma.