Habari Mseto

Washukiwa wa Anglo-Leasing wamshangaa DPP kuhusu ushahidi

May 29th, 2019 Kusoma ni dakika: 1

Na RICHARD MUNGUTI.

WASHUKIWA wa sakata ya Anglo-Leasing ambapo serikali ilipoteza zaidi ya Sh4.3 bilioni Jumatano walilalamika mahakamani kwamba Mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma (DPP) hataki kuwasilisha ushahidi kwamba kampuni ya Sunday Corporation iliwasilisha mitambo ya kiusalama waliyonunulia Idara ya Polisi miaka 16 iliyopita.

Wakili Ahmednassir Abdullahi anayewakilisha wakurugenzi wa kampuni ya Sunday Mabw Deepak Kamani, Rashmi Kamani na baba yao Chamanlal alishangaa sababu DPP ameendelea kuwasilisha ushahidi kwamba “bidhaa hazikununuliwa na kwamba Serikali ilipoteza pesa.”

“Mbona DPP hataki kuwasilisha ushahidi unaothibitisha bidhaa Serikali ilikuwa imeiomba shirika la Sunday Corporation inunulie idara ya polisi ziliwasilishwa nchini?” akauliza Bw Abdullahi.

Akimwonyesha hakimu mwandamizi Felix Kombo ushahidi wa Meli iliyowasilisha bidhaa hizo na tarehe zilizofika, Bw Abdullahi alishangaa sababu DPP ameendelea kuwasilisha ushahidi kwamba serikali iliporwa.

Wakili huyo alimkabidhi Bw Kombo barua iliyoandikiwa wizara husika na shirika la Sunday.

Wakili huyo alifichua hayo wakati wa kusikizwa kwa kesi ya ufisadi dhidi ya Deepak, Rashmi, Chamanlal , waliokuwa makatibu Dave Mwangi, David Onyonka na Joseph Magari.

Magari na Chamnlal waliruhusiwa na mahakama wasiwe wakihudhuria kesi kwasababu ya uzee.