Washukiwa wawili wa al-Shabaab waliovamia kituo wauawa Garissa, raia wanne waangamia
Na BRUHAN MAKONG
WASHUKIWA wawili wa al-Shabaab wameuawa, lakini raia wanne nao wakiangamia baada ya wapiganaji hao kushambulia kituo cha polisi Dadaab, Kaunti ya Garissa mapema Jumanne.
Bunduki mbili aina ya AK47 zimepatikana na pia vilipuzi viwili.
Kamanda wa Polisi katika eneo la Kaskazini Mashariki Paul Soi amethibitisha tukio hilo lililojiri saa nane na nusu usiku wa kuamkia Jumanne.
Aidha, wavamizi hao walikuwa wamelenga mtambo wa mawasiliano ulio katika eneo la Saretho, kaunti ndogo ya Dadaab.
“Ninathibitisha kwamba tukio hilo limejiri mapema Jumanne ambapo raia wanne wameangamia lakini muhimu ikiwa kwamba wapiganaji hao wawili wameuawa kwa kupigwa risasi,” amesema Bw Soi akiongeza kwamba walikuwa wanalenga kifaa cha mawasiliano cha kampuni ya Safaricom kabla ya ufyatuliamaji risasi.
Wahanga walikuwemo watoto ingawa hakuweka wazi ikiwa walikuwa wanafunzi.
Haya yanajiri siku mbili tu baada ya al-Shabaab kushambulia kambi ya wanamaji ya Manda-Magogoni, Kaunti ya Lamu ambapo mwanajeshi mmoja wa Amerika pamoja na wakandarasi wawili waliangamia.