Habari Mseto

Wataka mayai kutoka mataifa ya nje yapigwe marufuku Kenya

November 12th, 2020 Kusoma ni dakika: 2

Na LAWRENCE ONGARO

WAFUGAJI wa kuku Kaunti ya Kiambu wanaiomba serikali ipige marufuku mayai yanayoingizwa nchini kutoka nchi za nje.

Wakulima hao walisema mayai za bei ya nchini yamefurika nchini huku wafugaji wa humu nchini wakiachwa bila soko. Wafugaji wa kuku kutoka Gatundu Kaskazini na Thika magharibi ndio wameathirika zaidi na mpango huo.

Bi Nyambura Mwaura ambaye amefuga kuku 3,000 anasema kwa muda wa miezi sita iliyopita amepata hasara kubwa ajabu ambapo hajui la kufanya.

“Sisi wafugaji wa hapa nchini tuna uwezo wa kutosheleza mahitaji ya mayai lakini wafugaji wa nchi za nje wameharibu biashara kwa kiwango kikubwa. Tunaiomba serikali ifanye jambo ili kuokoa wafugaji hao,” alisema Bi Mwaura.

Wafugaji hao walisema mawakala ndio wameharibu biashara ya mayai hapa nchini na kwa hivyo ni sharti wakomeshwe kabla ya sekta ya ufugaji kuangamia.

Bi Mwaura alisema iwapo bidhaa zinazofurika humu nchini zitapigwa marufuku bila shaka wafugaji wa hapa nchini watafaidika na kujikimu vilivyo.

Walitaka serikali kuingilia kati na kukomesha biashara hiyo ambayo inaendeshwa na watu wenyewe ushawishi wa kibiashara.Wakulima hao walitaka serikali itoe hamasisho ili kuwapa wafugaji hao mwelekeo ufaao wa kukuza mayai yao.

Bi Beatrice Wangui ambaye ana zaidi ya kuku 2,000 anaofuga alisema ni vyema serikali iweke ushuru wa juu kwa wale wanaoingiza mayai hapa nchini.

“Tunaiomba serikali iwajali wafugaji wa hapa nchini kabla ya kuwakubali wafanyi biashara wa nje,” alisema Bi Wangui, na kuongeza hata tumekuwa tukiwapa majirani zetu mayai bure kwa sababu bidhaa hiyo imekosa soko.

Alisema wamelazimika kukuza mayai kwa bei ya kutupa nchini ya sh 10 jambo alilosema ni hasara kubwa kwa mfungaji.

Mbunge wa Thika Bw Patrick ‘ Jungle’ Wainaina, alikubaliana na matamshi ya wafugaji hao alisema tayari mswada wa mwaka wa 2018 wa kupiga bidhaa za kutoka nje marufuku iko bungeni na tayari imefika kiwango cha mwisho.

” Kulingana na msaada huo bidhaa zozote za kutoka nje zitalipa ushuru mara dufu kabla ya kukubaliwa hapa nchini. Kwa hivyo ikipita wafugaji watakuwa na jambo la kutabasamu tena,” alisema Bw Wainaina.

Ilidaiwa kuwa Kenya inaingiza bidhaa kutoka nje za takribani Sh 2 trilioni, huku ikituma bidhaa nje ya nchi kwa takribani Sh 500 bilioni kwa mwaka.