Watoto 20 wazaliwa Nakuru mkesha wa Mwaka Mpya
RICHARD MAOSI NA JOSEPH OPENDA
JUMLA ya watoto 20 walizaliwa katika mkesha wa mwaka mpya 2019 katika Hospitali ya Rufaa ya Nakuru.
Akina mama hao walipata zawadi ya mwaka mpya kati ya 12.00 -2.00 usiku kuamkia siku ya Jumanne na hawakuficha furaha yao .
Kulingana na nesi Beatrice Makhupe anayesimamia shughuli katika hospitali ya Nakuru Provincial General Hospital,Margret Kenyatta Mother Baby Wing anasema akina mama 14 walijifungua salama ilhali wengine sita walipata watoto wao kupitia njia ya upasuaji.
“Tumefurahia kupata zawadi ya mwaka mpya baada ya kuwasaidia akina mama kujifungua watoto 20 kwa muda wa saa 12 zilizopita.Bado tunachunguza hali zao na baadaye wakiwa katika hali shwari tutawaruhusu waondoke,”Makhupe alisema.
Kati ya watoto waliozaliwa wakiwa wazima 6 walikuwa ni wa kike na 8 wa kiume.
Joyce Mumbi mwenye umri wa miaka 19 alisema ni furaha tele baada ya kupata kifungua mimba wa kiume.
Kila mara alimtazama kwa furaha na kumpapasa mwanawe usoni akisema alikuwa tayari kutekeleza majukumu yake kama mzazi.
Alijifungua mkesha wa siku ya Jumanne na kumpatia jina Leon.
Mumbi anasema alikuwa ametembelea kliniki kuchunguza hali ya mtoto wake aliyekuwa hajazaliwa lakini daktari akamfahamisha alikuwa karibu kujifungua.
“Bila shaka ninamshukuru Mungu kwa kujaliwa mtoto wa kiume mwaka mpya, hii ni ishara nzuri kwa mustakabali wa maisha yangu,”Mumbi alieleza.
Akizungumza na Taifa Leo Digitali mzazi wa pili Bi Lucy Kabiru alijifungua mtoto wa kike na kumpatia jina Vennessa Njambi.
Alieleza kuwa Venessa Njambi ni mtoto alikuwa ni mtoto wake wa pili.
“Venessa amenipatia baraka ya mwaka mpya, ni jambo la kutia moyo mzazi kufungua mwaka kwa kujaaliwa mtoto,”alisema.
Akina mama hao hata hivyo walimiminia sifa tele usimamizi wa hospitali kwa kuwashughulikia vilivyo.
Aidha hatua ya Mama Margret Kenyatta kuanzisha hospitali hii imewasaidia akina mama wengi na kupunguza msongamano kwa hospitali ya Bondeni iliyokuwa ikitegemewa siku za mbeleni kutekeleza takriban kila kitu.
Mitambo ya kisasa,maji safi na huduma nzuri ni baadhi ya mambo muhimu yanayoshuhudiwa katika hospitali ya Margret Kenyatta Mother Baby Wing Nakuru.
Takriban watoto 395,072 wamezaliwa mwaka mpya 2019.Taarifa ya shirika la Umoja wa mataifa kushughulikia maswala ya watoto inasema asilimia 25 ya watoto waliozaliwa mwaka mpya ni kutoka bara Asia tu.
Mtoto wa kwanza duniani alizaliwa huko Fiji na wa Mwisho nchini Marekani kutegemea majira tofauti ya wakati ulimwenguni.