Watu 10 wanaswa kwenye msako dhidi ya karatasi za plastiki
Na CECIL ODONGO
SHIRIKA linalosimamia mazingira hapa nchini NEMA Jumatatu liliandaa msako wa ghafla kwenye soko maarufu la kuuza nyama la Burma jijini Nairobi ili kuwanasa watumizi wa mifuko ya plastiki iliyopigwa marufuku.
Msako huo ulihusisha maafisa wa shirika hilo na polisi wa Kituo cha Polisi cha Shauri Moyo wakiongozwa na OCS Bw Mark Odenyo.
Akizungumza na wanahabari baada ya operesheni hiyo, mkurugenzi mkuu anayesimamia mazingira kwenye shirika hilo kaunti ya Nairobi Bi Njoki Muriuki alilalamikia ongezeko la matumizi ya mifuko hiyo jijini.
Mwana mazingira huyo alisema kuwa japo marufuku hiyo iliasisiwa miezi mitano iliyopita, wafanyibiashara wadogo wadogo bado wameikaidi na kuendeleza matumizi yake kinyume cha sheria.
“Tumewanasa zaidi ya wafanyabiashara 200 kote nchini na tukiwafikisha mahakamani wengi wao hushindwa kulipa faini kati ya sh150,000 hadi sh300,000,” akasema. “Wakati huu hatutalegea na kutoka hapa tutaenda Gikomba na Muthurwa,” akaongeza.
Onyo
Bi Njoki alitisha kufunga soko hilo iwapo hali haitabadilika na kuongeza kwamba mifuko ya plastiki huingia humu nchini kiharamu kutoka Uganda, Tanzania na Somalia.
Wanabodaboda ndio hutumika sana na wanabiashara kufikisha mifuko hiyo bila kugunduliwa na maafisa wa usalama.
Wafanyibiashara kumi walinaswa kwenye msako huo na Jumanne walifikishwa kwenye Mahakama ya Kibera ili kujibu mashtaka ya kupatikana na bidhaa haramu.
Hali iligeuka tete wenzao walipowakabili wanahabari waliokuwa wakinasa tukio hilo na ikabidi maafisa waliokuwepo kukaa macho zaidi ili kuwalinda.
Habari za operesheni hiyo ilienea haraka mno sokoni na mara moja shughuli za kibiashara zikasimama wengi wakiyafunga maduka yao kutokana na hofu ya kukamatwa.
Waziri wa Mazingira na Maliasili Keriako Tobiko alitoa onyo kali kwa maduka ya jumla na wafanyibiashara kwamba sheria itawakabili vilivyo wasipotii marufuku dhidi ya mifuko ya plastiki.