Watu wanne washtakiwa kwa ulanguzi wa binadamu
Na RICHARD MUNGUTI
WASHUKIWA wanne wa ulanguzi wa raia 11 wa Ethiopia walishtakiwa Alhamisi katika mahakama ya Milimani jijini Nairobi.
Wanne hao Ali Matano Liban, Abdinassir Walde Baile, Mohammed Nakura Darchee na Mohammed Walde Haile walishtakiwa mbele ya hakimu mwandamizi Bernard Ochoi.
Walikanusha shtaka la kuwasafirisha raia 11 wa Ethiopia Mabw Melfin Melese, Adena Tergese, Adena Desita, Dersiene Ababba, Mesgne Live, Dawek Erebo, Daniel Basoro, Tamerat Daniel, Abirmhe Fordo, Abebe Metenso na Worku Wodmu.
Washukiwa hao kutoka nchi jirani ya Ethiopia walikamatwa Julai 9, 2019, eneo la Makuyu, Kaunti ya Murang’a.
Mahakama ilifahamishwa washtakiwa hao waliwasafirisha wageni hao ndani ya lori nambari ya usajili KBZ 577.
Ndani ya lori hilo, hakimu alifahamishwa, kulikuwa na sanduku maalum iliyokuwa imejengwa na kuwekwa ndani ya lori hilo kuonyesha lilikuwa linasafirisha mizigo.
“Polisi katika kizuizi cha Makuyu walisimisha lori muundo wa Hino na walipofungua sanduku kubwa lililokuwa ndani ya chuma waliwakuta raia hawa 11 kutoka Ethiopia,” kiongozi wa mashtaka alimweleza hakimu.
Mahojiano
Hakimu aliombwa awazuilie washtakiwa hao wanne katika kituo cha polisi cha Gigiri kwa mahojiano zaidi.
“Polisi kutoka kitengo cha uhalifu wa kimataifa kinachunguza ikiwa washtakiwa ndio wanaohusika na usafirishaji watu kutoka Ethiopia na kuwapeleka Afrika Kusini kupitia ama Uganda au Tanzania,” Bw Ochoi alifahamishwa.
Kiongozi huyo wa mashtaka alimweleza hakimu kuwa, idadi kubwa ya raia wa Ethiopia wamekuwa wakiingizwa nchini na makundi ya watu wanaoshiriki biashara ya kuwasafirisha watu hadi mataifa ya kigeni kufanya kazi huko.
Mahakama ilifahamishwa kuwa, washtakiwa hao hawakuweza kueleza walikuwa wanawapeleka wageni hao wapi lakini shtaka lilisema “walikuwa na nia ya kuwatumia vibaya.”
Hakimu aliamuru kesi hiyo itajwe leo ibainike iwapo itasikizwa Jumatatu kwa vile upande wa mashtaka uliomba mahakama ipokee ushahidi wa raia hao wa Ethiopia ndipo warudishwe makwao kwa vile itakuwa vigumu kuwaweka kwa muda mrefu humu nchini.
“Hii kesi itatajwa Ijumaa (leo) mkurugenzi wa mashtaka ya umma DPP aeleze idadi ya mashahidi alioorodhesha ndipo korti itenge muda wa kuisikiza mnamo Julai 15, 2019,” aliamuru Bw Ochoi.
Raia hao wa Ethiopia watazuiliwa katika kituo cha Polisi cha Gigiri nao washtakiwa hao wanne kutoka Kaunti ya Samburu watazuiliwa katika gereza la eneo la Viwandani, Nairobi.