• Nairobi
  • Last Updated May 4th, 2024 6:46 PM
Watu wengi hutumia maji ya Mto Athi bila kujua athari zilizopo

Watu wengi hutumia maji ya Mto Athi bila kujua athari zilizopo

Na BERNARDINE MUTANU

BW Vaati Mbiki, 35, anajitayarisha kuanza shughuli za kawaida za uvuvi katika Mto Athi.

Baada ya majaribio kadhaa, anafanikiwa kuwatega samaki wawili aina ya Mkunga, kama wanavyojulikana na wenyeji.

Hii ni shughuli muhimu kwake, kwani ndiyo anaitegemea kupata riziki. Bw Mbiki huwa anaendesha uvuvi katika Daraja la Miondoni, Kaunti Ndogo ya Mwala, Kaunti ya Machakos.

Amekuwa akijishughulisha na uvuvi kwa muda wa miezi kadhaa kufikia sasa, lakini samaki wamepungua maradufu.

“Wakati tulikuwa wadogo, tungewavua samaki kwa wingi sana lakini wamepungua sana nyakati za hivi karibuni,” akasema.

Anaeleza kuwa anadhani hali hiyo imechangiwa pakubwa na kiwango cha chini cha maji katika mto huo.

Ni mwezi Julai ambapo, kwa kawaida kiwango cha maji huwa juu. Hata hivyo, kiwango hicho kiko chini kiasi kwamba mtu anaweza kuvuka kutoka upande mmoja hadi mwingine wa mto huo bila kuogopa chochote.

“Kufikia mwezi Oktoba, kiwango cha maji kitakuwa chini zaidi. Kuna uwezekano kuwa huenda eneo hili likawa na matope pekee,” akasema.

Wakati wa mvua, maji huwa mekundu, kwa kuwa mchanga unaobebwa na maji huelekezwa katika mto huo.

Kwa sasa, haelewi sababu ya maji hayo kuwa yenye rangi ya kijani. “Kuna uwezekano kuwa rangi yake ni ya kibichi baada ya kuangukiwa na majani kutoka mitini,” akasema.

Wakati wa msimu wa kiangazi, hasa kati ya mwezi Agosti na Oktoba, maji hubadili rangi na kuwa ya kijani kutokana na kwekwe ambazo humea ndani yake.

Wakati ‘Taifa Leo’ ilipozuru katika eneo hilo, maji hayo yalikuwa yenye rangi ya kijani, huku yakitoa harufu mbaya kutokana na kwekwe hizo.

Kwekwe hizo pia huchangiwa na uwepo wa baadhi ya bakteria.

Kulingana na Shirika la Afya Duniani (WHO), baadhi ya bakteria hizo huwaathiri wanyama na mimea.

“Watu wanaweza kuambukizwa maradhihatari kwa kunywa ama kuoga kwa maji yaliyo na bakteria hizo. Athari mbaya zaidi za kiafya hutokea ikiwa mtu huweza kuyanywa maji hayo,” linasema shirika hilo.

Bw Mbiki anakubali kwamba Mto Athi ni kitegauchumi cha mamilioni ya watu wanaoishi karibu ama mbali nao.

Hata hivyo, alieleza kuwa hajui ikiwa maji hayo ambayo amekuwa akiyatumia yamejaa vimelea ambavyo vinaweza kumletea maradhi hatari.

Bw Mbiki hata hivyo anaonekana kutofahamu dalili ambazo anapaswa kuangalia ili kufahamu maji hatari kwa matumizi yake.

“Sijawahi kuathiriwa kwa vyovyote kwa kuyanywa ama kuyatumia kwa shughuli zingine. Ni vigumu kwangu kusema yana uchafu kwani nimeyatumia kwa zaidi ya miaka 30. Sijawahi kuwa mgonjwa. Mifugo wetu vile vile huwa wanayatumia na hawajawahi kupata maradhi,” akasema.

Cha kushangaza ni kuwa, Bw Mbiki na wenyeji wa eneo hilo huwa wanayanywa maji hayo bila kuyachemsha. Hii ni bila kujali dalili za wazi zinazoonekana kwamba maji hayo hayafai kwa matumizi ya binadamu.

Baadhi ya madhara ya bakteria hizo kwa mwanadamu ni mwasho wa ngozi, matatizo ya tumbo, kutapika, kuendesha, kuumwa na kichwa kati ya mengine.

“Wale wanaoogelea katika maji yenye bakteria hizo wanaweza kupata matatizo ya ngozi, ugonjwa wa pumu, matatizo ya macho, kujikuna na miasho katika mdomo na pua. Viumbe kama ndege na samaki pia wanaweza kupata madhara kutokana na bakteria hizo,” linaonya shirika hilo.

Vile vile, linaonya kuwa madhara hayo huenda yakawa mabaya sana, hasa kwa watoto.

Kulingana na Bw Patrick Luka, Mto Athi ni mfano wa eneo ambalo lilikuwa kitegauchumi kwa watu wengi, lakini sasa unahatarisha maisha yao.

Kulingana naye, maji hayo yalianza kubadilika miaka kumi iliyopita, kauli iliyoungwa mkono na babake na majirani wake kadhaa.

“Mwaka 2014 ndio ulikuwa mbaya zaidi. Tungepata maradhi ya ngozi yaliyotufanya kujikuna sana. Leo, wale wanaovuna mchanga wanapata maradhi kama hayo,” akasema.

Alieleza kuwa mara nyingi, wakazi huwa wanalalamika kuhusu maradhi kama homa ya matumbo, amoeba na ugonjwa wa kuhara, ambapo wanaoathiriwa sana ni watoto.

Shule zilizo katika eneo hilo huwa zinaelekeza maji zinayotumia katika mto huo.

“Mke wangu alipata homa ya matumbo na amoeba. Niligharamika sana kulipia matibabu yake. Baada ya utathmini wa kina, nilibaini kuwa ingenigharimu fedha nyingi zaidi ikiwa sote tungekuwa wagonjwa,” akasema Bw Luka.

You can share this post!

Wataka Rais atatue suala la mizigo SGR

Sh82 bilioni za ujenzi wa Bwawa la Thwake hatarini kupotea

adminleo