• Nairobi
  • Last Updated April 27th, 2024 6:00 PM
Watumiaji wa Thika Road eneo la Roysambu kuelekea Ruiru, Juja na Thika wahimizwa kutafuta njia mbadala

Watumiaji wa Thika Road eneo la Roysambu kuelekea Ruiru, Juja na Thika wahimizwa kutafuta njia mbadala

Na SAMMY WAWERU

MSONGAMANO wa magari unaendelea kushuhudiwa katika barabara kuu ya Thika Superhighway kufuatia ukarabati unaofanyika.

Hali hiyo inashuhudiwa kati ya mtaa wa Roysambu na eneo la Githurai, upande wa kuelekea Ruiru, Juja na Thika, katika barabara ya mwendo wa kasi.

Msongamano huo wa magari, hususan mchana, umeendelea kuonekana kwa muda wa siku tatu mfululizo zilizopita, kutokana na harakati za kuimarisha barabara hiyo chini ya Halmashauri ya Barabara Kuu Nchini (KenHA).

Alhamisi, hali hiyo ilianza kushuhudiwa asubuhi, huku ukarabati ukishika kasi. Matingatinga ya kuchanganya na kumwaga lami yanatumika kufanikisha shughuli hiyo.

“Tunahimiza watumizi wa Thika Road, wanaoelekea Githurai, Ruiru, Juja na Thika, watumie barabara ya nje (service lane) kwa sababu ya ukarabati unaoendelea,” mmoja wa afisa wa KenHA ameambia Taifa Leo.

Afisa huyo pia amependekeza madereva watumie Kamiti Road, barabara inayounganisha Roysambu, Kahawa West na Ruiru kuingia Thika Road ili kuruhusu ukarabati kufanyika.

Uimarishaji wa Thika Super Highway, hufanyika mara kwa mara, ili kudumisha sura ya barabara hiyo kuu nchini iliyoundwa chini ya serikali ya mseto, iliyoongozwa na Rais (Mstaafu) Mwai Kibaki na aliyekuwa Waziri Mkuu Raila Odinga.

Mwezi uliopita, Agosti, KenHA iliifunga (Thika Super Highway leni ya kasi, kati ya Garden City na Allsoaps) mara kadhaa ili kukamilisha utengenezaji wa madaraja ya watu eneo la Garden City na Allsoaps.

You can share this post!

Ibra apatikana na virusi vya corona

STEPHANIE MASEKI: Atumia tajriba ya uigizaji na filamu...