Habari MsetoSiasa

Wawili motoni kwa kurekodi safari ya usiku ya Uhuru na Raila

June 18th, 2020 Kusoma ni dakika: 2

Na RICHARD MUNGUTI

WAFANYAKAZI wawili wa hoteli ya New Stanley, Jumatano walishtakiwa kwa uhalifu wa kimitandao baada ya kudaiwa kufichua video iliyoonyesha Rais Uhuru Kenyatta na Kiongozi wa ODM Raila Odinga wakitembea katika barabara ya Kenyatta Nairobi usiku.

Endapo Patrick Rading Ambogo na Janet Magoma Ayonga watapatikana na hatia, watatozwa faini ya Sh10 milioni ama kusukumwa jela miaka mitano. Wawili hao tayari walisimamishwa kazi.

Rais Kenyatta na Bw Odinga walinaswa na kamera za CCTV za hoteli ya kifahari ya Stanley saa mbili na dakika 20 usiku wa Juni 2, 2020.

Washtakiwa hao wawili walikanusha mashtaka dhidi yao wakiwakilishwa na mawakili Apollo Mboya na Danstan Omari.

Bw Mboya anamwakilisha Ambogo naye Bw Omari anamtetea Bi Ayonga.

Mawakili waliomba mahakama wakabidhiwe taarifa za mashahidi wakiwemo Rais Kenyatta na Bw Odinga.

“Tunatarajia kupewa nakala za mashahidi wanaojumuisha Rais Kenyatta na Bw Odinga. Katika taarifa za hawa wanatakiwa kueleza ikiwa walinakiliwa na kamera za CCTV wakitembea usiku kati kati mwa jiji la Nairobi,” alisema Bw Omari.

Pia alisema video asili yapasa kuonyesha picha za Rais Kenyatta na Bw Odinga ndipo wathibitishe kwa hakika ni wao waliokuwa wakitembea katika barabara ya Kenyatta usiku wa Juni 2, 2020.

Mawakili hao walisema watapinga shtaka dhidi ya washtakiwa hao kwa vile halielezi ikiwa wawili hao walivuruga kompyuta na kunukuu picha za Rais Kenyatta na Odinga wakitembea mjini.

Wakiomba washukiwa hao wawili waachiliwe kwa dhamana mawakili hao walisema hoteli ya New Stanley iliwatimua kazi washtakiwa baada ya video hiyo kusambazwa katika mitandao ya kijamii.

Mabw Omari na Mboya walisema washtakiwa hao walikuwa wameachiliwa kwa dhamana ya Sh5,000 na polisi na kuagizwa wafike kortini kujibu shtaka.

Kiongozi wa mashtaka Bi Angela Fuchaka hakupinga ombi lao wakiachiliwa kwa dhamana. Hakimu aliwaamuru walipe dhamana ya Sh10,000.

Kesi dhidi yao itatajwa Julai 2 kwa maagizo zaidi. Pia hakimu aliagiza mawakili hao wapewe nakala za mashahidi pamoja na video iliyokuwa inasambazwa katika mitandao.

Video hiyo iliyosambazwa sana katika mitandao ya kijamii iliwaonyesha Rais Kenyatta na Bw Odinga wakikagua ukarabati wa barabara za katikati ya jiji kuu.

Ukarabati huo unaendelezwa chini ya Idara ya Usimizi wa Nairobi (NMS) ambayo iko chini ya Afisi ya Rais.