Wawili wajeruhiwa vibaya baada ya gari kubingiria mara kadhaa Lamu
Na KALUME KAZUNGU
WATU wanne walinusurika kifo pale gari dogo la mmiliki binafsi, walimokuwa wakisafiria, lilikosa mwelekeo Jumanne usiku na kubingiria mara kadhaa eneo la Mambo Sasa, karibu na mji wa Witu, kwenye barabara kuu ya Lamu kuelekea Mombasa.
Wanne hao ambao ni wahudumu wa afya wa serikali ya Kaunti ya Lamu, walikuwa wakisafiri kutoka Lamu kuelekea Mombasa pale dereva alishindwa kulidhibiti.
Walioshuhudia wamesema gari hilo lilipoteza mwelekeo ghafla barabara ambapo lilipinduka na kubingiria pembezoni mwa barabara hiyo.
Wawili kati ya abiria wanne waliokuwa ndani waliumia vibaya kichwani na miguuni na kupelekwa katika zahanati ya Witu ambapo baadaye walipewa rufaa ya matibabu kwenye hospitali ndogo ya Kaunti, mjini Mpeketoni.
“Gari lenyewe lilikuwa likiendeshwa kwa kasi mno. Ghafla dereva akashindwa kulidhibiti. Tuliona gari hilo likiacha barabara na kisha kubingiria,” akasema Bw Emmanuel Wanyoike.
Afisa Mkuu wa Polisi (OCPD) wa tarafa ya Mpeketoni, Harrison Njuguna, amethibitisha kutokea kwa ajali hiyo na kusema kuwa walioumia tayari wamepelekwa hospitalini na ambako wanaendelea kupokea matibabu.
Walioumia ni Mohammed Fatima Farouk ambaye ni dereva wa gari hilo na ambaye alilalamikia maumivu makali ya viungo muda mfupi baada ya ajali na Bi Jackline Mose ambaye ni muuguzi wa hospitali ya King Fahad mjini Lamu na ambaye alipata majeraha ya kichwa wakati wa ajali hiyo.
Wanusurika
Aidha Bw Abdi Bahola ambaye ni daktari kwenye hospitali ya King Fahad mjini Lamu na mwenzake Bi Hadija Athman walinusurika kwenye ajali hiyo bila majeraha yoyote.
“Ni kweli. Kumekuwa na ajali ya gari dogo la kibinafsi eneo la Mambo Sasa, karibu na mji wa Witu. Gari lilikuwa na watu wanne, akiwemo dereva. Lilikuwa likiendeshwa kwa kasi. Dereva alishindwa kulidhibiti, hivyo likabingiria mara mbili. Wawili walipata majeraha ya kichwa na viungo vingine vya mwili ilhali wengine wakinusurika ajalini bila majeraha yoyote.Walioumia walikimbizwa hospitalini eneo la Witu na Mpeketoni. Gari limeburutwa na kuwekwa kwenye kituo cha polisi mjini Witu huku uchunguzi ukiendelea,” akasema Bw Njuguna.
Afisa huyo aidha aliwashauri madereva wanaotumia barabara kuu ya Lamu kuelekea Mombasa kuwa makini zaidi hasa msimu huu ambapo mvua imekuwa ikinyesha na kusababisha utelezi barabarani.
“Kama mnavyofahamu, ujenzi wa barabara ya Lamu kuelekea Mombasa unaendelea. Sehemu nyingi bado ziko katika hali mbaya na zinateleza hasa msimu huu wa mvua. Madereva wawe waangalifu ili kuepuka ajali na hata kusababisha maafa barabarani,” akasema Bw Njuguna.