Wazazi waishtaki KNEC kufuta matokeo ya wanafunzi 125
Na RICHARD MUNGUTI
WAZAZI wa shule moja ya upili Kaunti ya Garissa wamelishtaki Baraza la Kitaifa la Mitihani (Knec) kwa kufutilia mbali matokeo ya kidato cha nne cha wanafunzi 125.
Kati ya wanafunzi 128, ni wanafunzi tu watatu ambao matokeo yao hayakufutiliwa mbali.
Wazazi 125 waliwasilisha kesi katika mahakama kuu wakiomba Knec ishurutishwe kubadili msimamo wake na itoe ushahidi jinsi wanafunzi walivyoiba mtihani.
Wazazi hao wanaomba mahakama kuu ishurutishe Knec kubatilisha matokeo ya wanafunzi 125 kutoka shule ya upili ya Ikhlas Intergrated iliyoko Garissa mjini.
Katika kesi iliyowasilishwa na Bw Abdirizak Omar Ibrahim kwa niaba ya wazazi wengine 124 mahakama imejulishwa kwamba Knec haikueleza sababu ya kufutiliwa mbali kwa matokeo hayo.
“Kati ya wanafunzi 128 ni wanafunzi watatu tu ambao matokeo yao yalitangazwa,” alisema Mwalim mkuu wa shule hiyo Bw Mohammed Abdi alipozugumza na Taifa Leo katika mahakama kuu Milimani.
Akiandamana na wanafunzi sita wanafunzi sita kuwasilisha kesi hiyo Mabw Abdi na Ibrahim walisema walifuata utaratibu waliopewa na Knec kusaka suluhu lakini hawakufanikiwa.
Knec iliandikia shule hiyo mnamo Desemba 21 2018 ikiieleza kuwa matokeo ya mtihani wa KCSE yamefutiliwa mbali kwa sababu ya undanganyifu.
“Tuliwasilisha rufaa kwa Knec lakini hatukufanikiwa,” alisema Bw Abdi.
Katika kesi hiyo mahakama imeelezwa kuwa wasimamizi wa shule hiyo walihakikisha kwamba mitihani imefanywa katika mazingira mazuri na kwamba “hakuna undanganyifu ulioendelea wakati wa mtihani wa kidato cha nne.”
Wazazi hao wamesema kwamba mnamo Januari 4 mwaka huu waliomba Knec ibatilishe uamuzi wake lakini ikakataa.
Mahakama imeratibisha kesi hiyo kuwa ya dharura na kuamuru Knec, Wizara ya Elimu na Mwanasheria mkuu wapewe nakala za kesi hiyo iliyowasilishwa na wakili Evans Mirieri wajibu sababu ya kufutiliwa mbali kwa matokeo ya shule hiyo.