Habari Mseto

Wazee sasa wamgeukia Mungu amalize njaa

February 26th, 2018 Kusoma ni dakika: 2

WINNIE ATIENO na PETER MBURU

HALI mbaya ya kiangazi na njaa imewalazimu wazee wa jamii ya Agikuyu kutoka Kaunti ya Nakuru kumgeukia Mungu kwa maombi, huku watoto wakiwa hatarini kufa kwa njaa kaunti ya Kilifi.

Mnamo Jumamosi, wazee hao walikusanyika eneo la Maili Sita, Bahati ambapo kwa njia za kitamaduni walifanya matambiko wakimlilia Mungu kumaliza janga la kiangazi.

Maombi hayo yalifanywa huku shirika la Msalaba Mwekundu likisema watu 241,000 wanahangaishwa na njaa, hasa katika kaunti za Kilifi, Tana River na Taita Taveta.

Ziara ya Taifa Leo katika Kaunti ya Kilifi ilionyesha Mto Sabaki umebadili mkondo wake, huku mabwawa manne pekee kati ya 25 yakiwa na maji ambayo yanang’ang’aniwa na mifugo na binadamu.

Meneja wa shirika la Msalaba Mwekundu eneo la Pwani, Bw Hassan Musa, alisema kuwa huenda hali hiyo ikawa mbaya hata zaidi kutokana na hali ya anga isiyotabirika.

“Katika Kaunti ya Taita Taveta takriban watu 77,000 wanakabiliwa na njaa, Tana River ni 35,000 na Kilifi 129,000. Kilifi ndiyo imeathiriwa zaidi haswa eneo la Magarini ambapo watu 51,000 wanapata taabu kwa sababu ya uhaba wa chakula na maji. Bamba-Ganze ni watu 41,000, Kaloleni 20,000 na Malindi 10,000,” Bw Musa alisema.

Waziri wa Maji, Misitu na Mazingira katika Kaunti ya Kilifi, Bw Kiringi Mwachitu, alisema kuwa wakazi wengi hujihusisha na biashara ya kuchoma makaa kwa sababu ya umaskini.

Katika kaunti hiyo, maeneo yaliyoathiriwa zadi na ukame ni Magarini na Malindi.

“Kwa sasa wakazi wa Bamba wana maji. Hata hivyo kuna changamoto za maji katika eneo la Magarini na Malindi na tunazishughulikia. Katika eneo la Ganze tumewekeza mno katika sekta ya maji,” akasema.

Hata hivyo Bw Musa ameitaka serikali kuwaelimisha wakazi kuhusu upanzi wa miti.

“Kiangazi cha muda mrefu kimefanya maji kuwa machafu. Wakazi wanatumia maji ambayo hayajatiwa dawa na pia wanalazimika kutumia maji hayo na mifugo,” akasema.

Hali hiyo ya kiangazi ni mbaya mno, kiasi kwamba baadhi ya wakazi wameanza kuathiriwa na ugonjwa wa ngozi, unaotokana na utapia mlo.