• Nairobi
  • Last Updated May 3rd, 2024 4:40 PM
Wazee sasa waongoza kwa uchezaji kamari – Ripoti

Wazee sasa waongoza kwa uchezaji kamari – Ripoti

Na VALENTINE OBARA

IDADI kubwa ya Wakenya wanaocheza kamari kila siku ni wazee wa zaidi ya miaka 55, utafiti wa Benki Kuu umeonyesha.

Hii ni kinyume na imani ambayo imekuwepo kwamba vijana ndio hucheza michezo hiyo ya bahati nasibu zaidi.

Utafiti huo uliofanywa kwa ushirikiano na Idara ya Takwimu za Kitaifa (KNBS) na shirika la Financial Sector Deepening (FSD) kote nchini, unaonyesha kuwa asilimia 33.2 ya Wakenya wenye umri zaidi ya miaka 55 hucheza kamari kila siku, ikilinganishwa na asilimia 20.6 pekee ya vijana wa kati ya miaka 18 hadi 25.

Vile vile, wachezaji kamari angalau kila wiki wenye kati ya miaka 18-25 ni asilimia 48.7, na wenye miaka 46-55 ni asilimia 57, huku kukiwa na asilimia 53.6 ya wenye umri kati ya miaka 36-45.

Kwa msingi huo huo, wenye miaka 18-25 wanaocheza kila mwezi ni asilimia saba pekee nao wenye umri wa zaidi ya miaka 55 ni asilimia 30.4.

Wiki iliyopita, Waziri wa Usalama, Dkt Fred Matiang’i alilalamikia idadi kubwa ya vijana ambao wametekwa na uchezaji kamari. Lakini utafiti huu unaonyesha kuwa wazee walio na zaidi ya miaka 55 ndio wanaohitaji kusaidiwa zaidi kutokana na uraibu huo.

Ripoti hiyo pia inaeleza kuwa hali ngumu ya maisha imewafanya Wakenya wengi kushindwa kulipa madeni yao “mama mboga” mitaan.

Utafiti uliofanywa na Benki Kuu ya Kenya ulipata kuwa mikopo ambayo haijalipwa kutoka kwa maduka hayo ya mitaani inaongoza kwa asilimia 45.4 kati ya madeni yote yaliyolemea Wakenya.

Sababu zilizotolewa na wengi walioshindwa kulipia mikopo hii ya bidhaa muhimu za matumizi ya kila siku ni kwamba walipatwa na dharura, walitumia fedha kulipia mikopo mingine, na wengine wakakiri hawakujipanga vyema kifedha.

Ripoti za hivi majuzi zimekuwa zikionyesha Wakenya wanazidi kulemewa na gharama ya maisha.

You can share this post!

Wameingia ‘box’ ya Jubilee?

Pombe kwa wenye njaa yazua ghadhabu

adminleo