Habari Mseto

Wazee wa Kalenjin wazidi kugawanyika kuhusu Ruto

June 12th, 2020 Kusoma ni dakika: 2

BARNABAS BII na ONYANGO K’ONYANGO

UTATA umezuka kuhusu hatua ya baadhi ya wazee wa Baraza la Wazee la Talai kumtawaza Naibu Rais William Ruto kama kiongozi wa kisiasa wa jamii ya Wakalenjin, baada ya kundi pinzani kupuuzilia mbali hatua hiyo.

Kundi hilo limedai kuwa kitendo hicho ni njama ya kumdharau Rais Uhuru Kenyatta na kushusha thamani ya utamaduni wa jamii hiyo.

Ijumaa, kundi la wazee wa baraza hilo limeonya kwamba huenda Dkt Ruto akapata laana, ikiwa hatatakaswa kwa kukiuka tamaduni za jamii hiyo.

Wazee hao wameongozwa na naibu mwenyekiti wa baraza hilo, Bw Christopher Koyogi.

Dkt Ruto alitawazwa rasmi kama kiongozi wa kisiasa wa jamii ya Kalenjin kwenye hafla iliyofanyika nyakati za alfajiri Ijumaa iliyopita.

Dkt Ruto pia alipata baraka kwenye nia yake ya kuwania urais mnamo 2022.

Wazee hao, ambao walifanya mkutano katika eneo la Kapsisiywa, Kaunti ya Nandi, walisema kuwa Rais Kenyatta bado ana vifaa maalum vya uongozi, hivyo hakuna mtu mwingine anayeweza kutawazwa kama kiongozi kabla yake kumaliza muhula wake uongozini.

“Rais Kenyatta aliomba baraka zetu ili kuendelea na uongozi wake baada ya kumaliza muhula wa kwanza kwenye hafla iliyofanyika katika eneo la Nandi Hills. Tulimpa vifaa maalum vya uongozi ambavyo anashikilia hadi sasa. Hivyo, ni makosa makubwa kwa baadhi ya wazee kumpotosha Dkt Ruto kwamba anaweza kuidhinishwa kama kiongozi wa Wakalenjin. Wazee hao pia walikiuka taratibu za kitamaduni za ukoo wetu,” amesema Bw Koyogi.

Vifaa maalum

Lakini kulingana na wazee wa ukoo huo, wakiongozwa Kasisi Mstaafu James Baasi, Dkt Ruto ndiye anayeshikilia vifaa maalum vya uongozi.

Vifaa hivyo, ambavyo ni mavazi maalum ni ‘Sambut’, ‘Kuutwet’, ‘Sharit’ na ‘Rungut.’ Dkt Ruto pia alipewa asali (Kumiat).

Alisema kuwa hilo ndilo linamfanya kuwa kiongozi wa jamii hiyo.

Kasisi Baasi, ambaye alihudumu katika Kanisa la Anglikana la Kenya (ACK), alisema kuwa Dkt Ruto ndiye kiongozi wa jamii hiyo sasa, na hakuna mtu mwingine anayeweza kukabidhiwa uongozi kwani kiongozi hutawazwa tu kwa wakati mmoja,

“Vifaa vyote ambavyo tulimpa Dkt Ruto mnamo Ijumaa vinaashiria masuala kadhaa. Kwa mfano ‘Sambut’ inaashiria uongozi wa pamoja, ‘Kutwet’ inaashiria mamlaka huku ‘Sharit’ ikiashiria mwongozo. Hivyo, hakuna mtu mwingine anayeweza kukabidhiwa vifaa hadi Dkt Ruto atakapomaliza muda wake wa uongozi,” akaelezea Bw Bassy.

Hata hivyo, wazee hao wamesema kwamba itambidi Dkt Ruto kushauriana na wazee wa jamii ya Nandi na wa ukoo wa Talai kutakaswa ili kuepuka mkosi.

“Itawabidi Dkt Ruto na washirika wake kufuata kanuni za kitamaduni zifaazo kwa kukutana na wazee wa Nandi na Talai ili kufanya hafla ya kumtakasa,” ameongeza Bw Koyogi.