• Nairobi
  • Last Updated April 27th, 2024 9:35 PM
Wazee wa vijiji wataka serikali iwape mishahara na sare za kazi

Wazee wa vijiji wataka serikali iwape mishahara na sare za kazi

Na Alex Njeru

WAZEE wa vijiji Kaunti ya Tharaka-Nithi, wameiomba serikali ya kitaifa kuwalipa mishahara na kuwapa sare za kazi.

Wakizungumza katika mkutano mjini Marimanti, eneobunge la Tharaka jana, wazee hao walisema wao ni sawa na watumishi wa umma wanaotekeleza jukumu katika utawala na wanafaa kutambuliwa.

Walisema wanafaa kuajiriwa na Tume ya Utumishi wa Umma na kulipwa mishahara kama wafanyakazi wengine wa serikali. Mmoja wao, Bw John Kimathi, alisema machifu na manaibu wao huwategemea kufahamisha umma mikutano na sera za serikali na kuwaeleza yanayoendelea vijijini.

“Sisi tunaunganisha watu na serikali na tunastahili mshahara hata kama ni kidogo wa kutukimu,” alisema Bw Kimathi.

Bi Mercy Mutegi, alisema wakati mwingine huwa watadhulumiwa na umma wakiwa kazini kwa sababu hawana sare za kazi au njia yoyote ya kujitambulisha.

Alisema serikali pia inapaswa kuwalipia bima ya matibabu akisema baadhi yao hawawezi kukimu mahitaji ya kimsingi.

“Tunaomba bunge kuweka sheria ambayo itafanya tutambuliwe kama wafanyakazi wa umma,” alisema Bi Mutegi.

 

You can share this post!

Waume waambia wenzao wakome kulamba asali kiholela

Serikali yaanza kulipa fidia wenye mashamba ya SGR

adminleo