Habari Mseto

Wazee waitaka NACADA kutuma kikosi kuzima uraibu wa mihadarati Lamu

November 30th, 2018 Kusoma ni dakika: 2

NA KALUME KAZUNGU

Wazee na viongozi wa kidini Kaunti ya Lamu wametamaushwa na ongezeko la vijana wanaotumia dawa za kulevya eneo hilo katika siku za hivi karibuni.

Wazee na viongozi hao wa kidini hasa wale wa kutoka miji ya Mtangawanda, Pate, Kizingitini, Faza, Mbwajumwali, Tchundwa na Myabogi, Kaunti Ndogo ya Lamu Mashariki na wale wa kisiwa cha Lamu, ikiwemo mitaa ya Kashmir, Bombay, Wiyoni na Kijitoni, Kaunti Ndogo ya Lamu Magharibi, wameeleza hofu yao kwamba ikiwa hatua za haraka hazitachukuliwa kudhibiti wanaosambaza dawa za kulevya eneo hilo, huenda Lamu ikakosa viongozi wa siku za usoni.

Katika kikao na wanahabari mjini Lamu Ijumaa, wazee na maimamu waliitaka Bodi ya Udhibiti wa Dawa za Kulevya nchini (NACADA) kutuma kikosi maalum eneo la Lamu ili kuwahamasisha vijana kujiepusha na ulanguzi wa dawa za kulevya.

Bw Alwy Salim alisema vijana wengi eneo hilo wameangamia kwenye janga la mihadarati, hatua ambayo pia imechangia wizi kuongezeka mitaani na vichochoroni.

Baadhi ya wakazi hasa kwenye mitaa ya Wiyoni, Mkomani, Kashmir na Bombay wamekuwa wakiporwa simu na fedha nyakati za usiku, uhalifu ambao unaaminika kutekelezwa na waraibu wa mihadarati.

“Kwanza tunalaani wale ambao wanasambaza dawa za kulevya eneo hili. Vijana wetu wameharibika ilhali wizi umeongezeka mitaani na hata majumbani. Tungeomba Bodi ya NACADA kuja Lamu na kushughulikia suala la dawa za kulevya. Limekuwa kero kwa vijana wengi na huenda tutakosa viongozi wa kesho endapo suala hilo halitadhibitiwa,” akasema Bw Salim.

Bw Kassim Shee kutoka Kizingitini alisema ni vyema kituo cha kurekebisha tabia kwa walanguzi wa dawa za kulevya eneo la Hindi kiharakishwe kufunguliwa ili vijana ambao tayari wamejitosa kwenye janga la mihadarati waweze kuokolewa.

Bw Shee alisema dawa za kulevya zimechangia vijana wengi kuacha masomo ili kuendeleza uraibu huo.

“Baadhi ya vijana wameacha shule ili kuendeleza uraibu wa dawa za kulevya. Kazi hawataki na ni hao hao vijana ambao wakiona kitu chochote wanaiba ili kuuza na kukimu kiu chao cha dawa. Kituo cha urekebishaji tabia kifunguliwe haraka ili kuokoa kizazi chetu,” akasema Bw Shee.

Ni hivi majuzi ambapo Shirika la Msalaba Mwekundu lilitangaza kwamba kituo cha urekebishaji tabia eneo la Hindi kingefunguliwa hivi karibuni hasa baada ya kukamilika kwa asilimia 95.

Kituo hicho kilichojengwa chini ya ufadhili wa shirika hilo kiligharimu jumla ya Sh 75 milioni.

Kituo hicho kina uwezo wa kupokea takriban waathiriwa 100 wa dawa za kulevya kwa awamu moja.