• Nairobi
  • Last Updated May 17th, 2024 6:50 AM
Waziri aitunuka sifa Kisumu kwa kiwango cha juu cha usafi

Waziri aitunuka sifa Kisumu kwa kiwango cha juu cha usafi

Na SAMMY WAWERU

KAUNTI ya Kisumu imepongezwa kwa kudumisha usafi katika kiwango cha hali ya juu.

Kati ya kaunti ambazo Waziri wa Afya Mutahi Kagwe amezuru kutathmini maandalizi katika kupambana na Covid-19, amesema Kisumu ndiyo inaongoza katika udumishaji wa kiwango cha usafi.

Hata ingawa Waziri anasema kila kaunti ina sifa yake ya kipekee na inayoifanya kuwa tofauti, alisema Kisumu imeonyesha ukakamavu kuhakikisha mazingira yake ni nadhifu.

“Mji wa Kisumu ni safi sana, mjivunie na muendelee vivyo hivyo,” Bw Kagwe akasema, akieleza kwamba alikaribishwa na taswira ya mazingira safi na yaliyomridhisha.

Waziri alisema hayo Jumapili baada ya kuzuru kaunti hiyo kutathmini maandalizi yake katika kukabiliana na corona.

Alisema picha iliyomlaki Mjini Kisumu, inaashiria wakazi wanathamini usafi, akieleza udumishaji usafi ni mojawapo wa kigezo kinachohitajika kupambana na ugonjwa wa Covid-19.

“Usafi ni kati ya mahitaji tunayotilia mkazo katika vita dhidi ya corona. Wakazi wa Kisumu, ninawapongeza. Kuna kaunti zingine ukitembea hujui iwapo uko kwenye msitu au la,” waziri Kagwe akaelezea.

Wizara ya Afya imekuwa ikilalamikia utupaji maski kandokando mwa barabara na njia, na pia kwenye dampo kiholela, suala linalohatarisha maisha ya wakazi kuambukizwa virusi vya corona ikiwa waliokuwa wamezivalia wameambukizwa virusi hivyo hatari.

Miezi kadhaa iliyopita serikali kuu ilizindua mpango wa Kazi Mtaani, ambao jukumu la walioajiriwa ni kuimarisha kiwango cha usafi nchini.

Aidha, mradi huo unajumuisha vijana walio kati ya umri wa miaka 18 – 35, na ambao wameathirika kufuatia janga la Covid-19, Waziri Kagwe akisema serikali itaendelea kuwafadhili ili waweze kujiendeleza kimaisha na kukimu mahitaji ya kimsingi.

Programu ya Kazi Mtaani imeajiri zaidi ya vijana 270, 000 kote nchini, ambapo wanapokea mshahara wa Sh455 kila siku.

Mpango huo unahusisha kufyeka nyasi kandokando mwa barabara, kwenye njia na pia mitaani. Vilevile, vijana waliopata ajira wanazoa taka, na shughuli zingine za kusafisha mazingira kwa jumla.

You can share this post!

UDAKU: Kipa mkongwe Neuer kanasa kimanzi tineja

Kundi lawapa vijana mafunzo kama njia mojawapo ya kuzuia...

adminleo