Habari Mseto

Waziri Alice Wahome augua, akosa kufika Seneti kujibu maswali

Na COLLINS OMULO October 30th, 2024 Kusoma ni dakika: 2

WAZIRI wa Ardhi na Ujenzi Alice Wahome Jumatano alifeli kufika katika Seneti kujibu maswali yaliyoelekezwa kwa wizara yake, baada ya kuugua.

Spika Amason Kingi alisema Waziri huyo alikuwa ameratibiwa kufika mbele ya maseneta katika kikao cha asubuhi lakini “macho yake yakafura kiasi cha kutoweza kuona vizuri”.

Bw Kingi aliwaarifu maseneta kwamba Bi Wahome alifanyiwa upasuaji wa macho siku tatu zilizopita na akaanza kuhisi nafuu lakini hali yake ikawa mbaya zaidi Jumatano asubuhi.

Waziri wa Elimu Julius Ogamba pia alikuwa ameratibiwa kufika Seneti kujibu maswali ambayo maseneta walielekeza kwa wizara yake.

“Tuliwatarajia mawaziri wawili katika kikao cha asubuhi ili wajibu maswali. Hata hivyo, nimepokea barua kutoka kwa Waziri wa Ardhi kwamba hangeweza kufika katika kikao cha leo kujibu maswali yaliyoelekezwa kwa wizara yake kwani anaugua,” Bw Kingi akasema.

“Nilizungumza kwa njia ya simu na Katibu wa Wizara hiyo na ananielezea shida yake. Waziri alifanyiwa upasuaji siku tatu zilizopita na alikuwa amehiari kufika leo. Lakini aliamka macho yake yakiwa yamefura tena. Hawezi kuona vizuri na hiyo ndio maana ameomba radhi kuwa hatakuwa nasi leo,” akaongeza.

Kwa hivyo, Spika Kingi aliahirisha kutolewa kwa majibu ya maswali yote yaliyoelekezwa kwa Wizara ya Ardhi.

“Hii ni sababu yenye mashiko na hivyo tumeahirisha maswali yote ambayo Waziri Wahome aliratibiwa kujibu,” akaeleza.

Bi Wahome alikuwa ameratibiwa kujibu maswali kuhusu sababu zilizochangia kuchapishwa kwa tangazo kwenye gazeti rasmi la serikali, kujulisha umma kuhusu wizi wa hatimiliki 367 za ardhi.

Aidha, alitarajiwa kufafanua kuhusu kutolewa kwa taarifa na wizara yake kuelezea hizo zilikuwa karatasi za maalum za kuchapisha stakabadhi hizo, wala sio hatimiliki halali ziliibwa.

Swali hilo, ambalo liliulizwa na Seneta Maalum Hamida Kibwana, pia lilimtaka Waziri Wahome kueleza mikakati ambayo serikali imeweka kuhakikisha hatimiliki zilizopotea hazitumiwi kinyume na sheria.

Aidha, Bi Kibwana alitaka Waziri Wahome kueleza usaidizi ambao serikali itatoa kwa watu watakaoathiriwa endapo wakora watatumia hati kama hizo.

Seneta huyo pia alitaka Waziri kuelezea hatua ambazo serikali imechukua dhidi watu ambao waliruhusu wizi wa stakabadhi za umiliki wa ardhi.

Aidha, kulikuwa na swali kuhusu hatua ya serikali kutwaa ardhi kwa lazima kwa matumizi ya utekelezaji wa miradi ya umma na endapo wenye ardhi hizo wamelipwa fidia au la.

Swali hilo liliulizwa na Seneta Maalum Beatrice Ogolla.

Imetafsiriwa na CHARLES WASONGA