• Nairobi
  • Last Updated May 13th, 2024 7:55 AM
Wenye magari ya uchukuzi waagizwa kuweka orodha ya abiria wao

Wenye magari ya uchukuzi waagizwa kuweka orodha ya abiria wao

Na CHARLES WASONGA

SERIKALI imewataka wahudumu wa magari ya uchukuzi wa umma, na hasa ya masafa marefu, waweke rekodi za abiria wote wanaoyatumia nyakati zote.

Katibu wa Wizara ya Uchukuzi na Miundomsingi Charles Hinga amesema Alhamisi rekodi hizo zitasaidia kufuatilia kwa karibu visa vyovyote vya maambukizi ya virusi vya corona endapo vitaripotiwa.

“Vilevile, ninawahimiza wahudumu wa magari ya uchukuzi wa umma kuhakikisha kuwa magari yao yananyunyizwa dawa na abiria wanapewa jeli spesheli ya kusafisha mikono yao vizuri,” akasema.

Bw Hinga amesema hayo alipozindua kampeni ya kudumisha usafi katika vituo vya magari ya uchukuzi jijini Nairobi.

Kampeni hiyo ilizinduliwa katika Kituo cha Mabasi cha Kencom, katikati mwa jiji la Nairobi na imeshirikisha maafisa kutoka Wizara ya Afya.

Bw Hinga pia ametoa wito kwa madereva na utingo kuzingatia masharti kuhusu usafi kama vile uoshaji wa mikono.

Katibu huyo wa wizara amewataka wananchi kukoma kufanya safari zisizo na maana, ambazo alisema zinachangia kuenea kwa virusi vya corona.

Mnamo Jumatano, Gavana wa Kisumu Peter Anyang’ Nyong’o aliamuru kwamba magari yote ya uchukuzi katika kaunti hiyo yaanze kuweke rekodi za abiria wote, kama sehemu ya mikakati ya kuzuia maambukizi ya virusi vya corona.

You can share this post!

COVID-19: Visa vya maambukizi nchini vyasalia saba

Linah Anyango ateuliwa kuwania tuzo ya mwalimu bora duniani

adminleo