Habari Mseto

Weta apinga mpango kununua mahindi nje

April 6th, 2020 Kusoma ni dakika: 2

Na DENNIS LUBANGA

KIONGOZI wa chama cha Ford Kenya Moses Wetang’ula, amekashifu mpango wa serikali wa kununua mahindi kutoka nje ya nchi, akisema wakulima wana mazao ya kutosha kwenye maghala yao.

Seneta huyo wa Kaunti ya Bungoma badala yake aliitaka serikali itumie fedha hizo, kununua mahindi kutoka kwa wakulima akisema kwa sasa kuna mahindi ya kutosha nchini.

Wiki jana, serikali kupitia Wizara ya Kilimo iliidhinisha uagizaji wa magunia milioni nne ya mahindi kutoka nje, ikisema imechukua tahadhari ya mapema kuepushia taifa hili janga la njaa wakati huu virusi vya corona vinaendelea kutatiza nchi.

Hata hivyo, Bw Wetang’ula kwenye mahojiano ya kina na Taifa Leo, alisema kwamba serikali inafaa ifutilie mbali mpango huo na badala yake iwakwamue wakulima kwa kuyanunua mahindi yao.

“Ninafahamu kwamba wakulima wa mahindi katika kaunti za Trans Nzoia na Uasin Gishu pamoja na maeneo mengine nchini wana mahindi ya kutosha kutokana na mavuno ya msimu jana. Iwapo kuna pesa ya kuagiza mahindi kutoka nje, basi serikali inafaa ihakikishe kwamba inanunua mahindi kutoka kwa wakulima ili kuwaepushia hasara,” akasema.

Bw Wetang’ula pia alimtaka Waziri wa Kilimo Peter Munya kuhakikisha mahindi yote yanayohodhiwa na wakulima, yananunuliwa kabla ya mengine kuletwa kutoka nje ya nchi.

“Kununua mahindi ya wakulima kuwasaidia kupunguza mazao ili wajiandae na msimu wa upanzi unaokuja. Litakuwa jambo njema iwapo tutaagiza mahindi kutoka nje ya nchi baada ya kuyanunua magunia yote ya wakulima,” akaongeza.

Seneta huyo ambaye ni Naibu Mwenyekiti wa kamati ya seneti kuhusu kilimo, alishangaa kwa nini serikali iagize mahindi kutoka Mexico, Brazil ama Ukraine na kuinua kiuchumi wakulima wa mataifa hayo ilhali jasho la wakulima nchini lipotee na wazamie mahangaiko tele maishani.

“Nafaka na mahindi si vyakula pekee ambavyo serikali inafaa kununua kutoka kwa wakulima. Kuna mihogo, viazi vitamu na ndizi zinazoendelea kuoza mashamabani. Tunaomba serikali inunue mazao hayo na kuyasambaza katika maeneo ambayo yanakabiliwa na ukame ambako hakuna vyakula vya kutosha,” akasema.

Wiki jana waziri Munya alisema serikali itanunua magunia ya mahindi milioni mbili kutumika kama chakula na Wakenya huku mengine milioni mbili yakisagwa na kutumika kutengeneza lishe kwa mifugo.

“Ningependa kuwahakikishia Wakenya kwamba serikali imeweka mikakati ya kutosha kuhakikisha hakuna ukosefu wa chakula nchini. Serikali ya kitaifa na ile ya kaunti zinafanya kazi pamoja kuhakikisha inaimarisha sekta ya kilimo nchini,” akasema Bw Munya.