Habari Mseto

Wetang’ula apinga mkutano wa Ford Kenya ulioitishwa na Eseli

November 9th, 2020 Kusoma ni dakika: 1

Na Cecil Odongo

MZOZO wa uongozi ndani ya Chama cha Ford-Kenya unaendelea kutokota baada ya mrengo unaoongozwa na Seneta wa Bungoma Moses Wetang’ula kupinga kuandaliwa kwa Kongamano la Wajumbe mnamo Novemba 21.

Katibu Mkuu wa Ford Kenya Dkt Eseli Simiyu, ambaye ni hasimu wa kisiasa wa seneta huyo, alitoa notisi ya kuandaliwa kwa kongamano hilo ambalo linatarajiwa kurasimisha uongozi mpya ndani ya chama.

Hata hivyo, Bw Wetang’ula kupitia notisi iliyochapishwa kwenye gazeti moja nchini, aliwataka wanachama wa Ford Kenya wasusie mkutano huo, akisema Dkt Simiyu alifurushwa kama katibu mnamo Mei 31 na hana mamlaka ya kuitisha mkutano wowote wa chama.

“Dkt Simiyu hashikilii tena wadhifa wa katibu mkuu Ford Kenya na ni marufuku kwake kujishughulisha na masuala yoyote ya chama hiki. Pia mahakama ya Nairobi ilimzuia kuhusika au kuendesha suala lolote la chama hadi kesi iliyoko kortini isikizwe na iamuliwe,” ikasema notisi hiyo.

Aidha mrengo wa Bw Wetang’ula ulisisitiza kuwa kongamano hilo halikuidhinishwa na wanachama wa Ford Kenya au asasi zozote za uongozi wa chama jinsi alivyodai Dkt Simiyu kwenye notisi aliyotoa awali.

Ford Kenya imekuwa ikabiliwa na mzozo wa uongozi baada ya Dkt Simiyu na mbunge wa Kanduyi Wafula Wamunyinyi pamoja na wanachama wengine kutekeleza mapinduzi mnamo Mei 31 na kumwondoa Bw Wetang’ula kama kinara wa chama.