Wezi waliozoea kuhangaisha wakazi wateketezwa Valentino Dei
NA RICHARD MAOSI
WEZI watatu waliteketezwa hadi kufa katika eneo la Barnabas, Kaunti ya Nakuru Valentino Dei.
Washukiwa hao walikiri kuhusika katika misururu ya uhalifu inayoshuhudiwa mara kwa mara katika eneo hilo na kutatiza hali ya utulivu.
Kulingana na Joseph Maina ambaye ni mkazi, ahalifu hao wamekuwa wakihangaisha raia. Aidha alisifia hatua ya wananchi kuangamiza sehemu ya genge hilo.
“Hii sio mara ya kwanza kupata taabu mikononi mwa wahalifu, wanaotekeleza maovu peupe bila kuogopa idara ya usalama,” alisema.
Waendeshaji bodaboda pia walieleza kuwa masaibu waliyokuwa wakipitia, yalichangiwa na wahuni hao ambao huwashambulia wakiwa wamejihami.
Hasa wakati wa usiku ambapo maeneo mengine hayawezi kufikika kwa sababu ya utovu wa usalama.
Wakazi walinyoshea kidole cha lawama polisi na wamiliki wa maeneo ya burudani kwa kuwahifadhi majangili.
“Siku za hivi karibuni polisi wamepunguza kushika doria jambo linalowapa wahalifu mori ya kuendeleza uhuni bila kuhofia serikali,” Maina aliongezea.
Hili linajiri siku mbili tu baada ya mwendeshaji bodaboda kuuawa katika hali ya kutatanisha.
Bw Robert Muchiri babake mwendazake alielezea wasiwasi wa kumpoteza mwanawe kwa njia ya ukatili.
“Mwanangu alikuwa katika shughuli za kujitafutia mkate wa kila siku alipokumbana na mauti,”alisema.
Alieleza kuwa raia wenye hasira walilazimika kuzima uhalifu,ingawa mikakati ya mazishi kumzika mwanawe ilikuwa ikiendelea.
Kufuatia kisa hicho msongamano mkubwa wa magari ulishuhudiwa katika njia ya Nakuru-Nairobi.
Juhudi za kupata habari zaidi kutoka kwa OCPD wa Nakuru Samwel Obara hazikuzaa matunda kwani hakupokea simu zetu.