Wezi wavunja ofisi ya shule na kuiba vipakatalishi vya wanafunzi
WANAFUNZI wa shule ya Kegati DEB Comprehensive School iliyoko Nyaribari Chache, Kaunti ya Kisii wanakabiliwa na mashaka baada ya wezi kuiba vifaa 28 vya kielektroniki ambavyo wamekuwa wakitumia kusomea.
Watu wasiojulikana wanasemekana kupata nafasi ya kuingia kwenye chumba ambamo vifaa hivyo vimehifadhiwa kwa kuvunja milango miwili ya chuma Jumatano usiku na kutoweka na vipakatalishi hivyo.
Bw Philip Ratemo, mwalimu wa miaka mingi shuleni humo alisema waligundua kuwa hali haikuwa shwari Alhamisi asubuhi walipowasili kwa masomo.
“Tuligundua kuwa ofisi zetu zilikuwa zimevunjwa tuliporipoti kazini. Milango ya mahali pa kuhifadhia vifaa vyetu ilikuwa wazi na tulipoingia tuligundua kuwa vifaa vya kielektroniki ambavyo tulipewa na serikali havipo. Tumeripoti suala hilo kwa polisi,” Bw Ratemo alisema.
Mwalimu huyo aliongeza kuwa mlinzi wa shule hiyo aliwaambia kuwa hakuona wakati wezi hao waliingia shuleni.
“Tuna mlinzi ambaye alikuwa zamu usiku. Lakini tulipomuuliza iwapo alifanikiwa kuwaona waliovunja, alituambia kuwa hakusikia chochote,” aliongeza
Kamanda wa Polisi wa Kaunti Ndogo ya Kisii ya Kati Isaac Kimwele, aliongoza timu ya wapelelezi kuzuru shule hiyo kutathmini hali ilivyo.
“Kwa sasa hatuwezi kusema mengi lakini tumeanzisha uchunguzi wetu. Maafisa wa Idara ya Upelelezi wa Jinai (DCI) wanashughulikia suala hilo,” kamanda huyo wa polisi alisema na kuondoka haraka alipoona wanahabari wamefika shuleni.