Habari Mseto

WHITNEY VIREGWA: Usimdharau kwa mwili wake

March 6th, 2019 Kusoma ni dakika: 2

NA JOHN KIMWERE

NINA imani nitafika mbali katika uigizaji. Haya ni matamshi yake Whitney Viregwa akikiri kwamba tayari Kenya inazidi kupiga hatua katika tasnia ya filamu.

Mwigizaji huyu maarufu kama Queen anasema ingawa hajakomaa kwenye uigizaji, amepania kuwa miongoni mwa wenzake watakaobadilisha tasnia ya filamu nchini kuifikisha ngazi ya kimataifa.

Bila shaka wengi wanapokutana naye kwa mara ya kwanza watamdharau maana ana mwili mdogo kwa kutofahamu yeye ni mwigizaji, mwandishi wa filamu, mwogozaji wa filamu, meneja wa uzalishaji filamu pia mwanamuziki chipukizi.

”Nalenga kufikia hadhi ya kimataifa katika masuala ya uigizaji,” alisema binti huyu mwenye umri wa miaka 23. Ingawa alijiunga na uigizaji mwaka 2013 mwaka uliyopita alichanguliwa naibu mwenyekiti katika kundi la waigizaji wa humu nchini liitwalo Jambo Wood.

”Kupitia mwavuli wa Jambo Wood tunaamini taifa hili litafikia viwango vya nchi zinazofanya vizuri katika uigizaji ikiwamo Nigeria na Afrika Kusini. Ubinafsi, ulaghai wa maarifa na ukosefu wa mtaji ni baadhi ya sababu ambazo hudidimiza sekta ya uigizaji hapa Kenya,” alieleza.

”Katika uigizaji ningetaka kujituma kadiri ya uwezo wangu ili kubobea kufikia kiwango cha Gilbert Lukaku na Reuben Odanga wa humu nchini,” alisema na kuongeza kwamba hao humtia motisha zaidi. Katika kitengo cha mwongozaji wa filamu na uzalishaji huvutiwa nao David Flitcher na Kevin Spacey mtawalia wote wa Hollywood.

Kwa kuandika matini ya filamu anataka kujibiidisha kuhakikisha anatinga kiwango cha mwigizaji Stephen King wa Hollywood.

Anawachana waigizaji chipukizi nchini kwa kutotilia maanani kukuza talanta zao mbali kufikiria ujira kutokana na kazi ya uigizaji wao.

Katika utangulizi wake alifanya kazi na Prince Cum Media alipohusika kuzalisha filamu moja iliyokwenda kwa jina The Politician pia alifanya kazi na Hope Risers alipokuwa akifundisha wasanii chipukizi masuala tofauti katika uigizaji.

Tangia mwaka jana msichana huyu anafanya kazi na kampuni ya African Motion Pictures inayomilikiwa na Emma Kibunja. Kwenye brandi hiyo wanashughulikia filamu ya TV-Series iitwayo ‘Skwota,’ wanayoamini itapata soko na kupangawisha wengi tu siyo hapa nchini pekee mbali pia kimataifa.

Binti huyu siyo mchoyo wa mawaidha kwa waigizaji chipukzi. Anafunguka kwamba tasnia ya filamu inalipa vizuri lakini ni muhimu kwanza waigizaji chipukzi wafanye utafiti vyema, wajitolee kutazama filamu za wenzao pia wasome zaidi kuhusu taaluma hiyo bila kuweka katika kaburi la sahau kuwa wavumilivu.

Kama mwanamuziki msichana huyu ni mshirika wa 63 Band ambayo hutumbuiza wapenzi wa muziki wa burudani kwenye kumbi tofauti nchini.

”Binafsi ninalenga kuanza kughani tambo zangu baada ya miaka miwili ijayo maana najifunza masuala tofauti katika muziki,” alisema.

63 Band imefanikiwa kutunga zaidi ya nyimbo 20 zikiwamo:’Mishumaa,’ ‘H-Town Love,’ ‘5 Words,’ ‘Liar,’ na ‘Dunia’ kati ya nyingine.