• Nairobi
  • Last Updated April 28th, 2024 8:50 AM
WHO yaonya huenda Afrika ikawa kitovu cha maambukizi ya Corona

WHO yaonya huenda Afrika ikawa kitovu cha maambukizi ya Corona

JUMA NAMLOLA na MASHIRIKA

SHIRIKA la Afya Duniani (WHO) limeonya kuwa, bara la Afrika litaathiriwa zaidi na maambukizi ya virusi vya corona.

Jana pekee, zaidi ya watu wapya 500 waliambukizwa katika mataifa ya Afrika, huku Kenya ikitangaza kuwa watu 12 zaidi wameambukizwa virusi hivyo.

Waziri wa Afya, Bw Mutahi Kagwe, alisema kati ya 12 hao, watano ni wafanyikazi wa hoteli.

“Hatujakamilisha saa 24 lakini kati ya vipimo 450 tulivyochunguza, watu 12 wameathiriwa. Hii sasa inafikisha idadi ya watu waliopatikana kuwa na virusi vya corona Kenya kuwa 246,” akasema.

Bw Kagwe alikuwa akizungumza katika uwanja wa ndege wa Jomo Kenyatta, Nairobi, ambapo alisema kinachohitajika sasa ni uwezo wa kupima watu wengi zaidi. Kuathiriwa kwa wahudumu kama wa hoteli, kunatilia nguvu onyo la WHO, kwa kuwa ni vigumu kujua mhudumu mmoja alikutana na wateja wangapi hotelini.

Ingawa awali kulikuwa na dhana kuwa watu weusi ni sugu dhidi ya corona na wangeweza kuhimili maambukizi ya virusi hivyo, sasa imethibitika kuwa kinyume kwani kufikia jana, idadi ya walioambukizwa barani ilikaribia watu 20,000 na vifo zaidi ya 1,000.

“Kinachotia hofu ni kuwa, kinyume na awali ambapo maambukizi yalikuwa kwenye miji mikuu, sasa hivi yanaeleake mashambani, ambako hata kuwafikia watu kwa wakati mmoja inakuwa vigumu,” Mkurugenzi wa WHO barani Afrika, Dkt Matshidiso Moeti, aliliambia shirika la habari la BBC.

Alitoa mfano wa nchi za Afrika Kusini, Nigeria, Ivory Coast, Cameroon na Ghana ambako maambukizi yameshuhudiwa yakitokea zaidi katika miji iliyo mbali na miji mikuu.

Hali si tofauti hapa Kenya, ambapo kaunti za mbali na Nairobi na Mombasa zimeanza kushuhudia visa vya corona. Kwa mfano Mandera, Siaya, Nyeri, Vihiga na hata Laikipia zimeathiriwa.

Dkt Moeti alisema mataifa mengi ya Afrika, mbali na kukosa uwezo mkubwa wa kupima, hayana uwezo wa kuwatibu watu wanaoambukizwa.

“Muhimu kwa sasa ni kujaribu kupunguza uwezekano wa kuwepo wangonjwa wanaohitaji huduma muhimu kama vile kuwekwa kwenye mitambo ya kuwasaidia kupumua.,” akasema.

You can share this post!

Polisi wazidi kukaidi amri za kafyu

Msipore fedha za corona – Weta

adminleo