Wito mataifa yote yafunge biashara ya bidhaa za wanyamapori
PSCU na LEONARD ONYANGO
MKEWE Rais, Bi Margaret Kenyatta amehimiza jamii ya kimataifa kushinikiza kufungwa kwa masoko ya pembe za ndovu, vifaru na bidhaa nyinginezo zinazotokana na wanyamapori ili kupunguza visa vya uwindaji haramu.
Bi Kenyatta alisema vita dhidi ya uwindaji haramu havitafaulu ikiwa baadhi ya nchi zitaendelea kuruhusu biashara ya bidhaa zinazotokana na wanyamapori.
“Hatutafaulu kukabiliana na uwindaji haramu ikiwa masoko yanayochochea uovu hayatafungwa,” akasema mkewe Rais alipokuwa akihutubu katika makao makuu ya Shirika la Wanyamapori (KWS), Nairobi wakati wa hafla ya kuwatuza maafisa ambao wamefana katika uhifadhi wa wanyamapori.
Kulingana na KWS, visa vya uwindaji haramu wa vifaru vimepungua kwa asilimia 90.
Maafisa kadhaa wa Shirika la KWS walitunukiwa tuzo kutokana na juhudi zao za dhati katika kuhifadhi wanyamapori.
Maafisa wa KWS waliofariki wakiwa kazini pia walikumbukwa kwa juhudi zao.
Majina ya waliotuzwa wakiwa marehemu yalisomwa katika vitengo tofauti wakiwemo wale waliouawa kwa kupigwa risasi katika makabiliano na wawindaji haramu; wale waliouawa wakiwa kwenye majukumu ya kufanya uchunguzi; wale waliozama majini na wale waliofariki katika ajali za barabarani au angani wakiwa kazini.
Waziri wa Utalii Najib Balala alisema watoto wa mashujaa wanaopoteza maisha yao wakiwa kazini wanastahili kuajiriwa katika Shirika la KWS.