Wito Nakuru ipandishiwe hadhi kuwa jiji
Na ERIC MATARA
GAVANA wa Nakuru Lee Kinyanjui ametetea juhudi zake za kutaka mji wa Nakuru upandishwe hadhi na kuwa jiji.
Chama cha Wenye Viwanda (KAM) walipinga wito wa kutaka Nakuru kugeuzwa jiji huku wakisema kuwa mengi yanahitaji kufanywa kabla ya mji huo kupandishwa hadhi.
Wafanyabiashara hao waliokuwa wakizungumza walipokutana na maafisa wa serikali ya kaunti wiki iliyopita, walimtaka Gavana Kinyanjui kuboresha miundomsingi kama vile barabara, mifereji ya maji taka, taa, kushughulikia tatizo la maji kati ya mambo mengineyo kabla ya kutaka mji huo kufanywa jiji.
Wafanyabiashara hao wakiongozwa na msemaji wao Bi Perris Mbuthia walisema mji wa Nakuru unakumbwa na uhaba wa nyumba za makazi kutokana na ongezeko la watu.
Wafanyabiashara pia walisema mji huo hauna vifaa vya kukabiliana na mikasa ya dharura.
Lakini jana, Gavana Kinyanjui alisisitiza kuwa mji huo umehitimu kupandishwa hadhi licha ya kuwepo kwa changamoto hizo.
Bw Kinyanjui aliambia Taifa Leo kuwa changamoto hizo zitashughulikiwa baada ya mji huo kupandishwa hadhi kuwa jiji.
“Changamoto zilizoorodheshwa na wafanyabiashara ni kweli zipo lakini hata jiji la Nairobi halina kila kitu. Mji huu ukifanywa jiji tutaanza mikakati ya kuweka miundomsingi inayohitajika,” akasema Bw Kinyanjui.
“Mji wa Nakuru ukipandishwa hadhi kuwa jiji basi itakuwa habari njema kwa wakazi na wafanyabiashara. Serikali yangu imekuwa ikijitahidi kuboresha miundomsingi,” akaongezea.
Alisema serikali yake imeanza mchakato wa kuongeza idadi ya barabara na kuboresha miundomsingi mbalimbali kwa lengo la kufanya mji huo kuwa kivutio kwa wawekezaji.