Wito serikali iongeze maabara za nyama
Na RICHARD MAOSI
WATAALAMU katika sekta ya ufugaji wameitaka serikali iwekeze zaidi katika ujenzi wa maabara za kuchunguza ubora wa nyama.
Akizungumza katika warsha kuhusu ajira katika sekta nzima ya ufugaji, Profesa Erastus Kang’ethe, ambaye ni mtaalam wa lishe bora, aliomba serikali pia kuajiri wataalamu wa kutosha ili wasaidie kuelimisha jamii kuhusu mbinu bora za ufugaji na lishe bora.
“Hili litamsadia raia kufahamu mengi na kufanya uamuzi sawa inapohitajika,” akasema.
Aliongezea kuwa ingawa kuna sheria nyingi za kukinga wafugaji dhidi ya madalali bandia, bado kuna changamoto hususan kuhusu kuwepo kwa maabara na wataalamu wa kutosha.
Alisema ikiwa changamoto hizo zitatatuliwa, itasaidia taifa kuhimili ushindani mkali katika sekta ya nyama kutoka nchi za nje, ambapo mataifa kama vile Namibia, Tanzania na Ethopia yameshika kasi.
“Itakuwa ni afueni kubwa ikiwa serikali itasaidia kutoa mpangilio maalum wa utaratibu wa kufuata kuanzia hatua ya kulisha mifugo, kuchinja, kupakia na kutafuta soko kwa wafugaji,” akaeleza.
Warsha hiyo ya siku mbili ilikamilika wikendi katika mkahawa wa Great Rift Valley Lodge, Naivasha.
Hafla hiyo iliyoanza Ijumaa, iliwaleta pamoja wasomi, wataalam wa mifugo, wanahabari, mashirika ya Kenya Market Trust (KMT), Kenya Meat and Livestock Exporters Industry Council (KEMLEIC) na The Retail Trade Association of Kenya (Retrak).
Bw Wario Bonaya ambaye ni meneja wa Kenya Market Trust, alisema mifugo ina umuhimu mkubwa katika mchakato mzima wa kuhakikisha serikali inatimiza ajenda ya kuzalishaji chakula cha kutosheleza wananchi wake, kwenye Ajenda Nne Kuu zake kabla ya 2022.
Alisema uzalishaji wa chakula cha kutosheleza mahitaji ya umma ni muhimu kwa uchumi wa nchi, ambapo wadau wanastahili kuangalia matumizi na manufaa ya chakula.
Aidha alisema Kenya inatumia hela nyingi kufanya utafiti kuhusu maradhi ya mifugo ambayo yanaweza kuzuilika.
Meneja huyo wa KMT alihoji kuwa wafugaji wengi humu nchini wanastahili kupewa mafunzo ya kutosha ili kuimarisha mazao ya mifugo wao, hususan jinsi ya kudumisha usalama wa nyama ya mifugo.
“Baadhi ya nyama zinazouzwa mtaani huwa ni za bei nafuu isipokuwa sio salama kwa matumizi ya binadamu,” akaonya.
Vile vile, alilaumu wafanyabiashara wanaotumia njia za mkato kuuza nyama nchini kwa lengo la kujitajirisha haraka, bila kuzingatia afya ya umma.
Bw Bonaya alisema Kenya ina soko kubwa la nyama hasa misimu ya sherehe, na hivyo sekta hiyo inaweza kutoa nafasi nyingi za ajira kwa vijana, wafugaji na wasafirishaji wa mifugo na bidhaa za nyama hadi masoko ya humu nchini na pia ya kanda ya Afrika Mashariki.