Wito serikali kuu isitishe uuzaji viwanda vya miwa
DENNIS LUBANGA na BARNABAS BII
VIONGOZI kutoka maeneo ya kukuza sukari katika ukanda wa Magharibi, wanaitaka serikali kusimamisha ubinafsishaji wa viwanda vya sukari katika eneo hilo kutokana na matatizo ya kifedha na kiusimamizi yanayovikumba viwanda hivyo.
Badala yake, wanataka kushirikishwa kwa washikadau wafaao, ili kuimarisha utendakazi wa viwanda hivyo. Walisema kuwa wanataka kuhakikisha kwamba wakulima wa miwa wamepata soko nzuri kwa mazao yao na watakuwa wakilipwa kwa muda ufaao.
Wakiongozwa na Seneta Moses Wetang’ula wa Bungoma, viongozi hao walisema kuwa kuharakishwa kwa mchakato huo huenda kukakosa kutatua changamoto zinazowakabili wakulima.
“Ni sikitiko kwamba kamati ambayo imepewa jukumu la kuviuza viwanda vya sukari, ikiwa ni pamoja na kiwanda cha Nzoia, inafanya hivyo bila kuwashirikisha viongozi ambao ni wawakilishi wa wakulima,” akasema Bw Wetang’ula.
Spika wa Seneti Kenneth Lusaka, aliushinikiza usimamizi wa Kampuni ya Sukari ya Nzoia kuharakisha ulipaji madeni inayodaiwa na wakulima.
“Ni sikitiko kwamba kampuni hii inaendelea kusaga miwa na kuwauzia wafanyabiashara lakini haiwalipi wakulima. Lazima mtindo huu ubadilike ikizingatiwa kuwa kampuni ina usimamizi mpya,” akasema Bw Lusaka.
Kumekuwa na madai kwamba wasimamizi wa awali katika kiwanda hicho walikuwa wakiwalipa wafanyabiashara waliokuwa wakikiuzia bidhaa kwanza kabla ya wakulima. Kumekuwa na madai kuwa wafanyabiashara hao walikuwa wakitoa hongo kwa wasimamizi hao ili kulipwa kwanza.
Gavana wa Bungoma Wycliffe Wangamati aliitahadharisha serikali kuu dhidi ya kuharakisha mpango huo.
“Kama serikali za kaunti, tunapaswa kuruhusiwa kuwa na usemi katika mchakato wa uuzaji wa kampuni ili kuhakikisha kuwa vinawafaa wakazi,” akasema Bw Wangamati.
Gavana huyo na mwenzake Anyang’ Nyong’o wa Kisumu, waliiomba serikali kuu kuwashirikisha katika kutafuta suluhisho la kudumu kwa sekta hiyo.
Viongozi hao wawili waliiomba serikali ya kitaifa kuziorodhesha kaunti kuwa miongoni mwa wanunuzi wa kwanza, lakini izipe muda kulipa fedha zinazohitajika.