Habari Mseto

Wito vituo vya intaneti vianzishwe mashinani

October 1st, 2019 Kusoma ni dakika: 1

Na PHYLLIS MUSASIA

WIZARA ya elimu Nakuru, imeomba serikali ya kaunti ianzishe miradi spesheli ya mitandao mashinani, ili kusaidia wanafunzi na vijana kupokea maelezo ya mitandao kwa urahisi.

Kulingana na waziri wa Elimu Bw Joseph Kiuna, mambo mengi yamezidi kuangaziwa katika hali tofauti ikilinganishwa na jinsi ilivyokuwa miaka ya awali na ndio maana kila mmoja anapaswa kusonga na kasi ya teknolojia mpya.

“Wakati huu tunajaribu kuangalia jinsi ambavyo kando na masomo ya darasani, wanafunzi waweze kutambua talanta zao na kuzitumikia ipasavyo,” akasema Bw Kiuna wakati wa mahojiano kuhusu ndoto, kazi na matarajio ya wanafunzi siku zijazo.

Bw Kiuna hata hivyo, aliongeza kuwa ni kupitia wepesi wa kutumia teknolojia ndipo vijana wengi wataweza kujifunza mambo muhimu wasioyajua, jinsi ya kutafuta soko kwa biashara zao na hata kupata kujua mengi kuhusu talanta walizo nazo.

Kiongozi huyo alisema kuwa maeneo ya mashinani ndio yaliyo na idadi kubwa ya vijana na kwamba itakuwa ni jambo la busara kwa serikali ya kaunti kuhakikisha kuwa wanafunzi wengi wananufaika na mradi huo unaopendekezwa.

Kulingana naye, maeneo ya miji pia yanahitaji miradi ambayo itaweza kutoa huduma za bure za mitandao ili kuwawezesha wakazi kutumia mitandao kwa uhahisi.

Bw Kiuna aliwasihi vijana kuepukana na matumizi mabaya ya mitando na badala yake kutumia nafasi hiyo kujinuifasha na kuendelea maishani.

Alitoa mfano wa maswala ya kilimo kama mojawapo ya miradi ambayo inaogopwa sana na vijana wengi kwani wengi hukosa kutilia maanani kilimo kama kitega uchumi.