Habari Mseto

Wizara mbioni kuchunguza dhuluma Nairobi School

July 9th, 2019 Kusoma ni dakika: 2

NA MARY WANGARI

Kisa kuhusu mwanafunzi wa shule ya upili ya Nairobi School aliyedhulumiwa na viranja kiasi cha kufanyiwa upasuaji wa kichwa kimechukua mkondo mpya huku maafisa wa Wizara ya Elimu wakiandaa kikao cha dharura na usimamizi wa shule mnamo Jumanne.

Mkutano huo uliohusisha maafisa wanne wa Tume ya Kuwaajiri Walimu (TSC) waliandaa kikao cha faragha ambacho wanahabari walizuiliwa kukaribia majengo ya shule.

Kulingana na duru zilizotufikia, upasuaji wa mvulana huyo ulikuwa ukiendelea lakini hazikufichua ni katika hospitali ipi, ama kiwango cha jeraha.

Kisa cha mvulana huyo wa kidato cha pili mwenye umri wa miaka 15 aliyepigwa vibaya na viranja kiliwaacha Wakenya vinywa wazi baada ya kuangaziwa na kituo kimoja cha habari humu nchini mnamo Jumatatu, Julai 7.

Kulingana na mamake aliyechelea kutajwa, mwanafunzi huyo alionekana kuchanganyikiwa, alikuwa akivalia taulo (diapers) na hata hangeweza kuwatambua wadogo wake.

“Namtazama mtoto wetu na siwezi amini jinsi Nairobi School ilivyomtendea ukatili. Inabidi tumwangalie hata akila na kusugua meno. Nilienda kumchukua nikapata akiwa amepoteza idadi kubwa ya sare zake, mchafu na aliyejiwachilia,”

“Hata ameanza kujikojolea kitandani jambo ambalo hajawahi fanya. Ameenda kimya na hata hawezi kuwatambua viranja waliompiga. Ninahisi kuchoka sana na sina nguvu za kupigana sasa hivi. Acha tuangazie masuala ya afya kwanza. Tafadhali tuombeeni,” aliandika mama huyo katika kundi la Watsapp.

Mwalimu Mkuu wa shule hiyo alikanusha madai ya mtoto huyo kudhulumiwa na kusema alitibiwa katika zahanati ya shule na kisha wakawaita wazazi wake kumchukua hali yake ilipozidi kuzorota.

“Alikuwa ameonyesha dalili za unyonge na alijitenga. Alipokosa kipata nafuu wazazi wake waliitwa ili kumtafutia matibabu bora. Kwa ufahamu wa shule hakukuwa na ripoti ya yoyote ya dhuluma na tulifahamu tu kupotia mitandao ya kijamii,” alisema.

Ripoti ya daktari wa shule ilionyesha mvulana huyo alikuwa amepigwa mara kadha na alikuwa na maji kichwani hali inayoitwa Obstructive Hydrocephallus. Hali hii husababishwa na jeraha kichwani na dalili zake ni pamoja na kuumwa na kichwa, kukosa kutembea vizuri, kushindwa kuona, na tabia kubadilika.

Kulingana na daktari mvulana huyo alihitaji kufanyiwa upasuaji wa dharura ili kudhibiti hali yake pamoja na kufanyiwa ukaguzi zaidi.

Wazazi wa mvulana huyo walipotaja kwamba hawangemrejesha shule hiyo, ndipo alipofunguka na kusema kwamba kiranja mmoja alimzaba kofi na kumpiga kwa kukosa kujifunga tai akisema amekuwa akipigwa tangu kidato cha kwanza. Aliongeza kwamba mwanafunzi mwenzake alivunjwa mkono kutokana na kupigwa na viranja.

Kulingana na wanafunzi wenzake, tabia ya kijana huyo ilikuwa imebadilika katika siku za hivi majuzi.

“Angeenda kwa darasa lisilofaa na kukosa kuvalia sare kamili,” walisema.

Hata hivyo usimamizi wa shule ulikanusha madai hayo ukisema viranja wa shule huchaguliwa na wanafunzi.