Habari Mseto

Wizi wa majanichai shambani wakithiri

January 21st, 2024 Kusoma ni dakika: 2

NA RICHARD MAOSI

WAKULIMA wa chai katika Kaunti ya Kericho wanalalamikia wizi wa zao hilo, wahuni wakianza kuvamia mashamba yao na kuvuna kiungo hicho cha kinywaji.

Kero hiyo pia inaathiri kampuni zilizowekeza katika uzalishaji wa chai.

Visa hivyo vimeanza kuripotiwa chini ya mwaka mmoja tu tangu wafanyikazi wenye makazi maalum ndani ya mashamba makubwa ya kukuza majani chai kupoteza ajira.

Maeneo ya Chepseon, Ngoina Road, Kaisugu, Roret, Kabianga na Kapsoit yametajwa kuripoti idadi kubwa ya wizi.

Imebainika wahalifu wengi huwa wanashirikiana na mabroka ambao hununua kilo moja ya majani chai ghafi kati ya Sh40 na Sh60.
Aidha, msimu wa mvua nyingi ndio mashamba ya kibinafsi hupoteza mazao mengi kwa sababu wezi hujificha katikati ya migunda na kuendelea na ‘shughuli zao’.

Alfred Too ambaye ni mkulima wa kibinafsi wa majani chai katika eneo la Kabianga, anasema matatizo ya wakulima wengi yalianza 2018 baada ya mashine za kuchuma chai kuzinduliwa.

Hatua hiyo hata hivyo haikupokelewa vyema na wakazi wa Kericho, ikizingatiwa kuwa wengi wao wanategemea biashara ya kuvuna chai ili kujikimu kimaisha.

Majani chai kwenye shamba la mkulima Kericho. PICHA|SAMMY WAWERU

“Lakini hali ilizidi kuwa mbaya 2023 ambapo wafanyikazi zaidi walifurushwa, ikawalazimu kusaka ajira kwingineko baadhi yao wakirudi mashambani,” Too anasema.

Anasema malipo ya mabroka huwa ni ya papo hapo, jambo linalowavutia vijana kuingiza hela za haraka haraka.?

Soma pia https://taifaleo.nation.co.ke/habari/habari-za-kaunti/washukiwa-120-ndani-kwa-uchomaji-mashine-za-kuchuma-majani-chai

Mkulima Sally Chepchumba, ambaye ni mkazi wa Roret katika barabara ya Kericho -Ikonge anaomba polisi kujizatiti ili kunasa wahuni wanaotekeleza wizi wa chai.

Vilevile, anasema wakulima wengi wanakodolea macho lindi la umaskini, faida na bonasi zikiendelea kupungua.

“Baadhi yetu hatutapata bonasi za chai kwa sababu ya wezi ambao wamepunguza mazao,” Chepchumba anateta.

Juliet Adhiambo mkazi wa Nyagaco anasikitika akisema wafanyikazi wengi walisimamishwa kazi wakati ambao hawakuwa wakitarajia.

Adhiambo alikuwa akifanya kazi ya kuchuma majani chai katika Shamba la Unilever tangu 2021, ila anasema alipoteza ajira kama mchezo tu.

Anasema licha ya mzigo mzito wa gharama ya juu ya maisha, nafasi za ajira kwa vijana pia ni finyu, na hivyo basi serikali inapaswa kufikiria jinsi ya kuinua vijana.

Oktoba 2023, mashine za kuchuma chai ziliteketezwa na kundi la vijana wenye ghadhabu katika eneo la Chebown linalomilikiwa na wawekezaji wa kibinafsi Ekaterra.

Mashine hizo zilikuwa zikisafirishwa kuelekea shambani.

Hali kama hiyo ilishuhudiwa katika viwanda vya kuongezea chai thamani, ambapo majani chai na mitambo mingine iliibwa.