• Nairobi
  • Last Updated April 30th, 2024 1:01 PM
Wizi wa majeneza na misalaba makaburini washangaza wakazi

Wizi wa majeneza na misalaba makaburini washangaza wakazi

Na WAIKWA MAINA

WAKAZI mjini Ol Kalou, Kaunti ya Nyandarua wameshangazwa na visa vya wizi wa majeneza na misalaba katika makaburi ya umma eneo hilo.

Vile vile wamesikitishwa na kupuuzwa kwa mazingira ya makaburi hayo ambayo yako wazi na hayana usalama karibu na makao makuu ya Kaunti ya Nyandarua.

“Tunashuku kuna wezi wanaovamia makaburi usiku na kuiba majeneza na misalaba na kufanya matambiko. Mara kadhaa nimeona mwanga hafifu usiku kutoka makaburi hayo huku yale yaliyozikiwa majuzi tu ndiyo yakiwa yamesalia na misalaba. Mengine huwa yamefukuliwa na kujazwa mchanga nusu siku moja baada ya miili kuzikwa,” akasema mkaazi Michael Magu.

Bw Magu alisema amewahi mara nyingi kupata misalaba kadhaa imeng’olewa na kuwekwa katika kona moja ya makuburi kisha baadaye huwa inapotea katika hali isiyoeleweka.

Kulingana naye, misalaba ambayo hupotea sana ni ile iliyofukuliwa kutoka kwa makaburi yanayoaminika kuwa na majeneza ya bei.

Waziri wa Ardhi na Mipango katika Kaunti ya Nyandarua, Bw Lawrence Mukundi, aliahidi kwamba makaburi hayo yatazingirwa ua na kupandishwa hadhi hadi kiwango cha kisasa.

“Makuburi ni mahala pa mapumziko kwa wafu na ni vyema kuyang’arisha, kutoa ulinzi na huduma nyingine muhimu zinazostahiki. Itatuchukua miaka 20 kuyajaza kwa hivyo suala la upanuzi si muhimu lakini tutafanya hivyo ikiwa idadi ya vifo itaongezeka siku zijazo,” akasema Bw Mukundi.

Mkaazi mwingine Joseph Kamau alifafanua kwamba kuna visa ambavyo misalaba hubadilishwa na kuwekwa upya katika makaburi tofauti.

“Nilitambua hii baada ya mazishi ya jirani yangu wakati nilipata msalaba wenye jina lake katika kaburi tofauti,” akasema.

You can share this post!

Vijana wataka wabunge wapunguziwe malipo

Wabunge wa Jubilee waapa kumng’oa Rotich ofisini

adminleo