Habari Mseto

Wizi wa Sh72m: Korti kufanya maamuzi

September 10th, 2019 Kusoma ni dakika: 2

Na RICHARD MUNGUTI

MAHAKAMA itaamua Jumanne ikiwa washukiwa sita wa wizi wa Sh72 milioni za benki ya Standard Chartered watazuiliwa kwa siku saba au la.

Jana, Hakimu Mkuu wa Milimani, Nairobi, Bi Matha Mutuku, aliagiza kuwa washukiwa hao wapelekwe katika Hospitali Kuu ya Kenyatta wapomwe na kujua kiwango cha majeraha waliyopataka.

Washukiwa hao ambao miongoni mwao ni maafisa watatu wa Polisi wa Utawala, walidai kuwa walipigwa na kuumizwa. Wengine sita, wakiwa wafanyikazi wa kampuni ya G4S mnamo Ijumaa iliamuliwa kuwa wazuiliwe kwa siku tano katika kituo cha polisi cha Langata.

Konstebo Chris Machogu, Koplo Duncan Kavesa Luvuga, Konstebo Boniface Mutua, Vincent Owuor, Alex Mutuku na Francis Muriuki waliposhtakiwa jana, Kiongozi wa mashtaka Anderson Gikunda aliomba wazuiliwe kwa siku saba.

“Washukiwa walitiwa nguvuni Ijumaa usiku na Jumamosi. Polisi wanahitaji siku saba kukamilisha uchunguzi,” alisema Bw Gikunda.

Alisema polisi wanahitaji muda kuchunguza simu za washukiwa hao kubaini watu waliowasiliana nao.

Alisema pia polisi watachunguza kamera za cctv kuwatambua washukiwa wengine wanaoendelea kusakwa.

Wakili Cliff Ombeta alipinga ombi washukiwa kuzuiliwa kwa siku saba akisema walipigwa na kuumizwa vibaya.

“Koplo Luvuga alipigwa na kuumizwa na polisi. Aliumizwa kichwani, mikono na miguu. Polisi walimfunga mshukiwa huyu mikono na miguu. Alifungwa kando ya chumba cha mbwa katika kituo cha polisi cha Muthaiga.Alizamishwa ndani ya maji akiendelea kuhojiwa,” Bw Ombeta alimweleza Bi Mutuku.

Aliongeza kusema Owuor alipigwa na kudungwa vidole na kuwekwa pili pili akilazimishwa kusema yeye ni afisa polisi.

“Mshukiwa huyu sio afisa wa polisi. Mkurugenzi wa uchunguzi wa jinai (DCI) alidai mshukiwa huyu ni afisa wa polisi,” akasema.

Aliomba korti iwaachilie washukiwa hao waende hospitali kwa vile polisi hawatawapeleka.

“Usikubali ombi la polisi la kuzuiliwa kwa washukiwa hawa kwa siku saba.Huenda hautakuwa na washukiwa kabla ya siku hizo kukamilika,” alisema Bw Ombeta.

Alisena washukiwa watafia mikononi mwa polisi kulingana na mateso wamepitia. Aliomba korti iwape dhamana washukiwa wajipeleke hospitali.

Aliomba korti itupilie mbali ombi la upande wa mashtaka akisema ” hawajawasilisha ushahidi wowote kuwezesha mahakama kuwazuilia washukiwa.”

Wakili huyo alisema polisi walienda katika makazi ya washukiwa na kusababisha uharibifu mkubwa wakisaka pesa hizo.

“Polisi walirarua viti kupasua dari, walipasua magodoro na hata pilo wakitafuta pesa hizo,” Ombeta.

Hata hivyo hakimu aliombwa awazuilie washukiwa hao kwa vile wengine sita waliamriwa wazuiliwe kwa siku saba.