Wote 90,744 waliozoa C+ kwenda juu wahakikishiwa nafasi vyuoni
Na WANDERI KAMAU
WANAFUNZI wote ambao walipata alama ya C+ na zaidi katika mtihani wa Kidato cha Nne (KCSE) mwaka uliopita, watajiunga na vyuo vikuu vya umma na kibinafsi, Waziri wa Elimu, Amina Mohamed alisema Jumatano.
Hili ni kufuatia ripoti kwamba huenda wizara hiyo ikapandisha alama hiyo, hivyo kuwanyima nafasi baadhi ya wanafunzi 90,744 ambao walifuzu.
Ripoti zilisema kwamba serikali inapanga kuongeza alama hizo, baada ya kuibuka kuwa huenda ikakumbwa na changamoto katika kufadhili idadi kubwa ya wanafunzi ambao watajiunga na vyuo hivyo kupitia Halmashauri ya Kutoa Mikopo ya Elimu ya Juu (HELB).
Lakini akiwahutubia wanahabari jijini Nairobi jana, Bi Mohamed alisema kwamba Halmashauri ya Uteuzi wa Wanafunzi Watakaojiunga na Vyuo Vikuu na Vyuo vya Kadri (KUCCPS), tayari imeanza mchakato wa kuwafahamisha wanafunzi taasisi ambazo watajiunga nazo.
“Hakuna mwanafunzi aliyefuzu kujiunga na chuo kikuu atakayeachwa nje. Wote watapewa nafasi hiyo kulingana na mpango wa serikali kuhakikisha kwamba kila mwanafunzi aliyefanya mtihani wa KCSE atapata nafasi katika vyuo vikuu na vyuo vingine,” akasema.
Kulingana na utaratibu huo, wanafunzi 121,288 ambao walipata alama ya C na C- watajiunga na vyuo vya kadri kufanya diploma, 244,436 waliopata alama za D na D+ wataitwa katika taasisi za kiufundi kusomea kozi mbalimbali, sawa na wengine waliopata alama ya D- na E.
Jumla ya wanafunzi 631,750 walifanya mtihani huo.