Habari Mseto

Yafichuka Gavana Kihika amejifungua mapacha Amerika

Na MARY WANGARI March 26th, 2025 Kusoma ni dakika: 2

WABUNGE wanawake wamelalamikia ongezeko la dhuluma kidijitali dhidi ya viongozi wanawake hali inayokiuka haki zao kikatiba kama kina mama, wake na raia kibinafsi.

Viongozi hao wanaojumuisha wabunge, maseneta na wawakilishi wanawake walitangaza kusimama na Gavana Susan Kihika wakiwarai wakazi wa Nakuru na Wakenya kwa jumla kuwa na subra na mkuu huyo wa kaunti anayepata nafuu Amerika baada ya kujifungua mapacha.

Wakihutubia vyombo vya habari Jumanne, Machi 25, 2025 katika majengo ya bunge, walisisitiza kuwa viongozi wa kike vilevile hupitia matukio ya kimaumbile ikiwemo kujifungua, kunyonyesha na malezi na hawafai kamwe kushinikizwa kuchagua ama kuwa viongozi au kushughulikia matukio ya kibayolojia.

Viongozi hao akiwemo Seneta Mteule Tabitha Mutinda, Hamida Kibwana, Veronica Maina, aliyekuwa Seneta Mteule Millicent Omanga na Wawakilishi Wanawake Betty Maina na Cynthia Muge, walimpongeza Gavana Kihika wakisema amethibitisha wanawake wanaweza kuongoza na kuendelea kuchangia majukumu yao kijamii.

“Kama viongozi wanawake wa Kenya, tuko hapa kusimama na Gavana Kihika, mtumishi wa umma anayejituma na mama aliyewakaribisha mapacha duniani majuzi. Tunampongeza kwa kujifungua watoto wake. Ni baraka kutoka kwa Mungu na tunashukuru,” walisema kupitia taarifa ya pamoja.

Wakaongeza, “Tungependa kukumbusha umma kuwa uzazi ni mchakato wa kimaumbile ambao ni wa kipekee na kibinafsi zaidi. Kama viongozi wanawake, tunatambua changamoto za kipekee zinazoambatana na kusawazisha majukumu ya utumishi kwa umma na familia. Safari ya kuwa mama huleta furaha kuu lakini pia inaweza kuambatana na matatizo ya kiafya yasiyotarajiwa hivyo kuhitaji muda kupata nafuu na kuimarika kiafya. Wanawake wengi wamepitia haya na Gavana Kihika si tofauti.”

Seneta Kibwana alifafanua kwamba kando na kujifungua, wanawake hupitia changamoto mbalimbali hususan matatizo ya afya ya kiakili katika siku za mwanzo mwanzo.

“Gavana Kihika ni mama na sasa ni nafasi yake ya kuwa mama. Naomba Wakenya tumpe nafasi awe mama. Sisi kama wabunge tumemshikilia, Gavana Kihika ashikilie hapo,” alisema Seneta Kibwana.

“Kwanza tunafurahi, ameongeza idadi ya Wakenya. Tuna furaha sana kuwa na hao watoto. Tumpe nafasi yake. Kama Wakenya, wale wanaomkashifu, mnajua mwanamke akizaa huwa na matatizo ya afya ya kiakili. Kuna matatizo ambayo wanawake huendelea kupata. Lazima mtu apewe nafasi yake baada ya kujifungua, awe na nafasi ya kupumzika ili arudi kazini.”

Seneta Hamida alisema kama wabunge wanawake, “Tumesimama na Gavana Kihika na ukitaka kuongeza watoto wengine sisi tuko hapa.”

Waliwahakikishia wakazi wa Nakuru kwamba oparesheni za kaunti hazijakwama wakisema Gavana aliacha timu thabiti.

“Ametekeleza majukumu yake, ameacha timu ngangari iendelee kutekeleza majukumu yake kikatiba kwa watu wa Nakuru na tunawashukuru wakazi wa Nakuru, tunawaeleza hawakufanya uamuzi mbaya. Walifanya uamuzi bora zaidi na wataona matunda hivi karibuni,” alisema Bi Muge.

“Kwa wanawake wote, mnaweza kufanya yote, unaweza kuwa gavana, seneta, mwakilishi mwanamke, rais, waziri mkuu, waziri, unaweza kuwa chochote ulichowahi kuota na bado ufurahie kuwa mama.”