Yaibuka walimu wanatishwa wakubalie wanafunzi waibe KCPE na KCSE
Na STEVE NJUGUNA
VYAMA vya walimu vya KNUT na KUPPET vimetofautiana kuhusu madai kuwa walimu wanapokea vitisho ili washiriki katika wizi wa mitihani ya KCPE na KCSE.
Huku Kuppet kikishikilia kuwa baadhi ya wanachama wake wametishwa, kile cha Knut kimetaja madai hayo kama uvumi.
Kulingana na mwakilishi wa wanawake kitaifa katika KNUT, Bi Jacinta Ndegwa, chama hicho hakijapokea malalamishi ya vitisho kutoka kwa wanachama wake.
“Hakuna mwanachama yeyote wa Knut ameleta malalamishi kwetu ya kutishwa,” alisema Bi Ndegwa.
Hata hivyo aliitaka Tume ya Mitihani (KNEC) kupeleleza madai hayo.
“KNEC inafaa kupeleleza madai hayo. Walimu wetu wamewatayarisha wanafunzi vya kutosha na sidhani kuna yeyote ambaye anapanga wizi wa mitihani ama kushirikiana na yeyote katika wizi huo,” alisema alipokuwa akiwatubia walimu mjini Ol Kalou, Kaunti ya Nyandarua
Kwa upande wake, Kuppet kimewashauri walimu kupiga ripoti kwa polisi ikiwa watapewa vitisho vya kuwataka washiriki wizi wa mitihani.
“Tumegundua kwamba kuna watu ambao wamekuwa wakiwatisha walimu ikiwa hawatashirikiana nao kuiba mitihani. Tumewaambia wasitishwe na yeyote na ikiwa watapokea vitisho wapige ripoti kwa polisi,” alisema katibu wa Kuppet tawi la Laikipia, Bw Ndung’u Wangenye.
Alisema kuwa walimu hawatatumika kutekeleza wizi wa mtihani kwa vyovyote vile.
“Walimu hawatajihusisha na wizi wa mtihani. Wale ambao hutekeleza wizi huu wanajijua na wanafaa kutiwa mbaroni kwa mujibu wa sheria,” akasema Bw Wangenye.