Yaibuka wasichana wanakeketwa kisiri Samburu
Na GEOFFREY ONDIEKI
Juhudi za serikali na mashirika mbalimbali kumaliza ukeketaji wa wasichana katika kaunti ya Samburu zinaonekana kugongwa mwamba baada ya visa hivyo kuongezeka siku kumi zilizopita.
Inaarifiwa kuwa uovu huo hutekelezwa kisiri na kina mama wenye umri mkubwa vijijini.
Kwa sasa, polisi mjini Maralal wanawazuilia kina mama wawili kwa tuhuma za kumkeketa msichana mwenye umri wa miaka 14 kinyume na sheria. Inasemekana msichana huyo alipoteza fahama kwa zaidi ya masaa 18 baada kuvuja damu kupita kiasi, na hapo ndipo majirani walitoa habari kwa idara ya usalama.
Hata hivyo, polisi walifanikiwa kumnusuru msichana huyo na katika kumkimbiza hospitali kuu ya Maralal ambapo anaendelea kupata nafuu.
Kamanda wa polisi katika kaunti ndogo ya Samburu ya kati Bw Samson Rotich alisema kuwa msichana huyo alikatwa na kina mama wakongwe kijijini na walipashwa habari kutoka kwa umma wakati hali ya msichana huyo ilikuwa mbaya zaidi.
“Tulipata akiwa amefungiwa chumbani na hali yake alikuwa mbaya zaidi. Washukiwa tuko nao hapa na watashtakiwa kwa kosa hilo baadaye,” alisema.
Hata hivyo, idara ya usalama imeapa kuendelea kuwasaka wahusika wanaowakeketa wasichana wadogo. Bw Rotich alionya kuwa idara hiyo ya usalama ipo macho na inafanya kazi usiku na mchana ili kuangamiza uozo huo.
“Tunazidi kufanya kazi usiku na mchana na nahimiza umma kuripoti visa kama hivi kwa idara husika,” aliongeza.
Madaktari kutoka hospitali kuu ya Samburu waliambia Taifa Leo kuwa msichana huyo alikatwa vibaya na hivyo kupelekea kuvuja kwa damu zaidi.
“Alikatwa vibaya lakini sasa anapata nafuu hata ingawa anaonekana na unyonge kwa sababu kupoteza damu zaidi,” alisema Bi Lempushuna ambaye ni mhudumu wa afya.
Taifa Leo ilibaini kuwa msichana huyo, ambaye pia ni mwanafunzi wa shule moja katika eneo la Suguta , alikuwa tayari kuozwa baada ya kupitia kisu cha ngariba.
“Kufikia sasa kila kitu kilikuwa tayari. Kutoka hapa wazazi ilikuwa wapokee ng’ombe kadhaa kama mahari na kuanza mchakato wa kumuoza kwa lazima. Hiyo ndio mila yetu,”alisema mmoja wa wakazi ambaye aliomba jina lake lisitajwe