Habari Mseto

Yasikitisha Walibora hataona diwani yangu aliyoifasiri – Mshairi Abdilatif Abdalla

April 15th, 2020 Kusoma ni dakika: 2

NA ABDILATIF ABDALLA

MSHAIRI, MOMBASA

Nimezipokea hivi leo asubuhi habari za kifo cha Profesa Ken Walibora kwa masikitiko makubwa sana. Uhusiano wangu na Ken ni wa miaka mingi – tangu alipokuwa mwanafunzi Kenya, na baadaye Marekani.

Huko Marekani, Chuo Kikuu cha Ohio, ndiko alikoandika tasnifu yake ya shahada ya uzamivu, ambayo ilikuwa ni kuhusu diwani ya mashairi yangu, Sauti ya Dhiki, niliyoiandika gerezani; na pia diwani ya mashairi ya Alamin Mazrui, Chembe cha Moyo, aliyoiandika gerezani pia.

Mimi na Ken tulikuwa tukiwasiliana mara kwa mara, kwa sababu Ken hakuwa rafiki yangu tu, wala hakuwa mwenzangu tu katika shughuli zihusianazo na Fasihi na Lugha ya Kiswahili, bali alikuwa ni ndugu yangu, mdogo wangu. Siku zote akiniita “Kaka Abdilatif.” Kwa hivyo, katika msiba huu mmoja, kwangu mimi ni misiba mitatu!

Ken hakuwa msomi tu aliyebobea, hasa katika taaluma ya Fasihi, bali pia alikuwa ni mtu mwenye utu, jasiri, mnyenyekevu, asiyependa mbwembwe wala makuu; na siku zote alikuwa tayari kujifunza mapya, na akikubali kwa moyo safi kukosolewa anapokosea. Nayasema haya kutokana na uhusiano wangu binafsi mimi naye.

Mbali na riwaya zake kadhaa, na hadithi zake fupi; na mbali na hiyo tasnifu yake ya uzamivu na makala mbalimbali aliyoyaandika kuhusu maandishi yangu, vile vile Ken alijasiri kuifasiri kwa Kiingereza diwani yangu hiyo ya Sauti ya Dhiki; tafsiri ambayo imehaririwa na Dkt. Annmarie Drury, msomi anayesomesha Fasihi ya Ulimwengu katika Chuo Kikuu cha Queens, Marekani.

Yasikitisha sana kwamba hataiona tafsiri hii itakapochapishwa kitabu baadaye mwaka huu, kwa ushirikiano wa Chuo Kikuu cha Michigan, Ann Arbor, Marekani, na shirika la uchapishaji la Mkuki na Nyota, Dar es Salaam, Tanzania.

Mshairi maarufu wa Kiswahili wa karne ya 19, Muyaka bin Haji, alitunga akasema, “Ufapo ni lako jina, lipete wakumbukifu.”

Nina hakika jina la Ken Walibora litakumbukwa kwa miaka na mikaka katika mawanda ya taaluma ya Kiswahili. Buriani mwanaharakati mwenzangu wa Kiswahili, mwanataaluma na ndugu yangu, mdogo wangu. Umetutangulia! Nasi tuko njiani; katungoje!!

Taifa Leo Dijitali wiki hii itakuwa ikichapisha taarifa za wapenzi wa Kiswahili waliotangamana na nguli wa lugha Prof Ken Walibora, aliyefariki Ijumaa wiki iliyopita.