• Nairobi
  • Last Updated April 18th, 2024 9:15 PM
Zabuni zinazopewa wafisadi sasa zipewe walemavu – Wabunge

Zabuni zinazopewa wafisadi sasa zipewe walemavu – Wabunge

Wabunge Denita Ghati na David Sankok wakiwahutubia wanahabari katika majengo ya bunge Juni 5, 2018. Picha/ Charles Wasonga

Na CHARLES WASONGA

WABUNGE wawili maalum Jumanne wamezitaka wizara, idara na mashirika ya serikali kufanya biashara na kampuni zinazomilikiwa na walemavu, badala ya kampuni ambazo zinamilikiwa na matapeli.

Wakiwahutubia wanahabari Jumanne katika majengo ya bunge David Sankok (Jubilee) na Denita Ghati (ODM) walilalamika kuwa zaidi ya kampuni 150 zinazomilikiwa na watu wanaoishi na ulemavu ziliomba zabuni katika Shirika la Huduma za Vijana kwa Taifa (NYS) lakini wakanyimwa.

“Ni makosa sana kwa watu welamavu kunyiwa zabuni katika mashirika ya serikali kama NYS huku wakora waliowasilisha hewa wakipendelewa.

Tungependa kutangaza hapa kuwa wale kampuni zote zilipewa zabuni bandia katika NYS na kusababisha kupotea kwa Sh9 bilioni hazimilikiwi na watu hawa tunaowawakilisha bunge.

Wenzetu 150 waliomba biashara ya kuwasilisha bidhaa katika NYS walinyimwa licha ya kuwepo kwa sera ya serikali kwamba asilimia 30 za zabuni zitengewe akina mama, vijana na walemavu,” akasema.

“Hii ina maana kuwa walemavu sio wafisadi na hivyo wizara zote za serikali zinapasa kuwapa walemavu tenda ili kuokoa pesa za umma,” Bw Sankok akasema.

Naye Bi Ghati alisema Kenya inaweza kupiga hatua kubwa kimaendeleo ikiwa serikali itawapiga jeki watu walemavu kwa kuwainua kiuchumi.

“Kenya ina jumla ya walemavu 6.5 milioni, wengi wakiwa wamesoma zaidi lakini hawajapewa nafasi ya kunawiri. Tunaitaka serikali kuwatambua walemavu kwa kuwateua katika nyadhifa za juu serikali kando na kutoa zabuni kwa kampuni zao,” akasema Bi Ghati ambaye zamani alikuwa Mbunge Mwakilishi wa Kaunti ya Migori.

Bw Sankok na Bi Ghati waliielekezea kidole cha lawama Idara ya Mahakama wakidai ndio huhujumu vita dhidi ya ufisadi kwa kuwaachilia huru washukiwa.

“Ikiwa Jaji Mkuu Bw David Maraga aliweza kufutulia mbali matokeo ya uchaguzi wa urais mwkaa jana, mbona ameshindwa kuwazima wafisadi ambao wanapora pesa na rasimilia za taifa hili?” akauliza Bw Sankok.

“Maraga na watu wake ndio wanafaa kulaumiwa kwa zimwi la ufisadi unalizonga taifa hili. Wao ndio huachilia washukiwa wa wizi wa mabilioni ya fedha kwa misingi finyu ya kutopata ushahidi wa kutosha, ” akaeleza.

Hata hivyo, Bw Maraga aliahidi kuwa idara ya mahakama itashirikiana na matawi yote ya serikali katika vita dhidi ya ufisadi alipohutubu katika sherehe za Madaraka Dei katika Uwanja wa Kinoru, Meru.

Na mnamo Jumatatu Naibu Jaji Mkuu Bi Philomena Mwilu alisema majaji wataharakisha kesi za ufisadi zitakazofikishwa mbele yao.

You can share this post!

KIMYA CHA ‘BABA’: Raila aeleza sababu ya...

Ndege yatoweka angani katika milima ya Aberdares

adminleo