Habari MsetoSiasa

Ziara ya Raila nyumbani kwa Oparanya yaibua maswali

May 13th, 2019 Kusoma ni dakika: 2

BENSON AMADALA na CHARLES WASONGA

ZIARA ya kiongozi wa ODM Raila Odinga nyumbani kwa Gavana wa Kakamega imewaacha wengi na maswali baada ya viongozi hao kudinda kufichua masuala waliozungumzia.

Mnamo Jumapili Bw Odinga alimtembelea Gavana Oparanya nyumbani kwake eneo la Emabole, kaunti ndogo ya Butere katika kile kilichotajwa kama ziara ya kibinafsi.

Kiongozi huyo aliwasili kwa helikopta majira ya saa nne asubuhi kabla ya kufanya mkutano wa faragha na mwenyeji wake kwa takriban saa nne.

Baada ya mkutano, Bw Odinga na Gavana Oparanya walipiga picha pamoja lakini hawakufichua yale ambayo walijadili.

Kiongozi wa wengi katika bunge la Kakamega Joel Ongoro alisema viongozi hao wawili wajadiliana kwa muda pamoja kabla ya kuungana na wageni wengine ambao pia walifika katika makazi hayo.

“Ilikuwa ni ziara ya kibinafsi ya kiongozi wa ODM. Baada ya kukutana walitoka nje na wamekuwa wakizungumza na kufurahi pamoja,” akasema Bw Ongoro.

Baadaye Bw Odinga alishiriki chakula cha mchana na mwenyeji wake na wageni wengine.

Ziara ya Bw Odinga inajiri wakati ambapo Bw Oparanya amekuwa akisema kuwa anajiandaa kuwania urais 2022 baada ya kuhudumu kwa mihula miwili kama gavana wa Kakamega.

Awali, Oparanya ambaye pia ni naibu kiongozi wa ODM (wadhifa anaoushikilia pamoja na mwenzake wa Mombasa, Ali Hassan Joho) amekuwa akimtaka Bw Odinga kumuunga mkono, akisema amekuwa mwaminifu kwa kiongozi huyo wa ODM.

Kulingana na Bw Oparanya, uaminifu wake kwa Odinga ulidhihirika katika chaguzi za 2007, 2013 na 2017.

Aidha, ziara hiyo inajiri saa chache baada ya Bw Odinga kuwaambia wanasiasa wakome kumhusisha na kampeni za urais kuelekea uchaguzi mkuu wa 2022, akisema hajatangaza nia yake ya kuwania wadhifa huo.

“Mimi sijatangaza kuwa nitawania urais 2022. Na Rais Uhuru Kenyatta pia hajaniambia kuwa atawania tena. Lengo la muafaka wetu ni kuunganisha Wakenya pamoja kwa ajili ya maendeleo,” Bw Odinga akauambia ujumbe wa wazee kutoka jamii ya Agikuyu wanaoishi Rift Valley waliomtembelea nyumbani kwake Opoda Farm, Bondo, kaunti ya Siaya Jumamosi.

Majuzi tu, Bw Oparanya alikariri kuwa atawania kiti cha urais baada ya kukamilisha muhula wake wa pili na wa mwisho.

“Sasa ninajianda kwa kiti kikubwa nitakapomaliza muhula wangu wa mwisho kama gavana,” akasema alipohutubu kwenye mkutano wa hadhara katika kaunti ndogo ya Kakamega Kaskazini.

Lakini Bw Odinga hajawahi kumjibu kauli za naibu wake kuhusu ndoto zake za urais.

Juzi Bw Oparanya alikutana na wabunge kutoka kaunti ya Kakamega jijini Nairobi na akawahakikishia kuwa yu tayari kufanya kazi nao katika wadhifa wake kama Mwenyekiti wa Baraza la Magavana (CoG).

Mbunge wa Shinyalu Justus Kizito alisema walienda kukutana na Gavana Oparanya kumpa pongezi kwa kuchaguliwa kuwa mwenyekiti wa CoG ambapo walijadili masuala ya maendeleo “na sio siasa”.