Habari MsetoSiasa

Zogo lachacha Kuria na Duale wakikabana koo

February 13th, 2019 Kusoma ni dakika: 2

Na BENSON MATHEKA

KIONGOZI wa Wengi bungeni, Adan Duale na mbunge wa Gatundu Kusini Moses Kuria, wametofautiana vikali kufuatia madai ya Bw Duale kwamba chama cha Jubilee kitamtimua Kuria kutoka kamati za bunge.

Mnamo Jumatatu, Bw Duale alimlaumu Bw Kuria kwa kukaidi kanuni za chama na kumdharau Rais Uhuru Kenyatta na kuashiria kwamba chama tawala kitamchukulia hatua za kinidhamu.

“Bw Kuria amevuka mipaka na hatutakubali yeyote chamani kumdharau Rais. Kama chama, tutamchukulia hatua ili kudumisha nidhamu katika chama chetu,” Bw Duale alisema akiongea na runinga ya NTV katika ofisi yake.

Alisema chama hicho huenda kikamuondoa Bw Kuria kutoka kamati za bunge kama njia moja ya kumuadhibu kwa kukaidi kanuni zake. Alitaja matamshi ya Bw Kuria ya mkesha wa mwaka mpya alipomlaumu Rais Uhuru Kenyatta kwa kutelekeza eneo la Mlima Kenya kama yaliyonuiwa kumkosea heshima Rais kama kiongozi wa chama na kiongozi wa nchi.

Hata hivyo, Bw Kuria alimwambia Bw Duale kwamba haogopi kubanduliwa kutoka kamati za bunge.

“Kwanza, huna mamlaka ya kufanya hivyo. Hili ni jukumu la Katibu Mkuu Raphael Tuju na Kiranja wa Wengi Ben Washiali. Pili, sina shida kuondolewa kutoka kamati ya Uchukuzi na Bajeti mradi tu sheria ifuatwe,” Bw Kuria aliandika kwenye taarifa aliyosambaza kupitia mitandao ya kijamii. Bw Kuria ni naibu mwenyekiti wa kamati hiyo.

“Ninahudumu katika kamati hizi kwa hisani ya chama. Ikiwa chama kitaamua kwamba hakihitaji huduma zangu katika kamati hizi, nitatii,” alisema Bw Kuria.

Alimlaumu Bw Duale kwa kuhujumu miswada aliyodhamini mbunge huyo tangu 2014.

“Tatu, mateso haya yote siku moja yataisha. Umehujumu miswada yangu ya kibinafsi tangu 2014. Hakuna hata mswada wangu mmoja uliowasilishwa bungeni,” alidai Bw Kuria.

Alisema nia ya Bw Duale ni kuzima kamati ya bunge aliyopendekeza ya kuunga Waziri wa Usalama wa Fred Matiang’i katika majukumu yake ya kushirikisha kamati ya mawaziri kuhusu maendeleo iliyobuniwa na Rais Kenyatta.

Katika kile kinachoonekana kupanuka kwa mpasuko katika chama cha Jubilee kuhusu marekebisho ya katiba, Bw Kuria alimlaumu Duale kwa kumpiga vita kwa sababu ya kuunga kura hiyo.

“Fuata sheria na nitaondoka. Chukua nafasi zako katika kamati wakati wowote. Kuna majukwaa mengine mengi ninayotumia kuhudumia watu wangu,” alisema Bw Kuria.