Familia kadhaa zafurushwa kutoka kipande cha ardhi kinachodaiwa kumilikiwa na chuo kikuu
Na KALUME KAZUNGU
FAMILIA zaidi ya 10 zinahangaika bila makao Kaunti ya Lamu baada ya kufurushwa kutoka kwa kipande cha ardhi chenye ukubwa wa ekari 432 ambacho inadaiwa mmiliki ni Chuo Kikuu cha Egerton.
Familia hizo ambazo kwa sasa zimepiga kambi kandokando ya barabara katika eneo la Mikinduni, Wadi ya Mkunumbi, zimeitaka serikali ya kaunti na ile ya kitaifa kuingilia kati na kutatua mzozo huo.
Mnamo Desemba 19, 2019, familia hizo ziliachwa kwa mshangao baada ya maafisa wa polisi kuongoza shughuli ya ubomoaji wa nyumba zao na kisha kuwafurusha wakazi hao kutoka shamba hilo la chuo kikuu cha Egerton kwa madai kuwa maskwota hao walikuwa wamelivamia.
Msemaji wa maskwota hao, Joseph Kiplagat alisema licha ya wao kushinda kesi mahakamani miezi kadhaa iliyopita, ni jambo la kushangazwa kwamba serikali iliwafurusha kutoka kwa shamba hilo na kuwaacha bila pa kwenda.
“Mimi nimeishi na watoto wangu katika shamba hili tangu mwaka 2001. Inakuwaje leo hii tunafurushwa kwa lazima? Hatuna pa kwenda na familia zetu zinahangaika hapa kandokando ya barabara. Tunataka haki itendeke,” akasema Bw Kiplagat.
Joshua Yeri ambaye ni baba wa watoto wanane anasema ameishi kwenye shamba hilo tangu mwaka 2003.
Bw Yeri anasema licha ya kujiendeleza kwenye shamba hilo, serikali haijatambua maendeleo yao na badala yake iliwafurusha bila huruma.
Alisema ipo haja ya serikali kuwahamisha kwenye makao mbadala na pia kuwafidia hasara itokanayo na ubomozi uliotekelezwa Desemba, 2019.
“Njaa inatukumba hapa kwani chakula chote tulicholima kilikuwa hakijavunwa mashambani mwetu. Wametufurusha na mahindi yetu wameyazingira ua ndani ya shamba wanalodai kumilikiwa na chuo cha Egerton. Watufidie hasara ya mimea yetu na pia nyumba zote zaidi ya 50 walizobomoa kwenye ardhi husika. Pia watupe makao mbadala,” akasema Bw Yeri.
Bi Margaret Kamande ambaye ni mama wa watoto 12 na ambaye ameishi ndani ya ardhi ya Egerton kwa zaidio ya miaka 18 alisema kufurushwa kwao ghafla kutoka kwa shamba hilo kumeathiri masomo ya watoto wao moja kwa moja.
“Shule zimefunguliwa lakini watoto wetu hawawezi kuhudhuria masomo kutokana na kwamba hawana makao maalum. Tunaishi barabarani ambapo kuna mbu. Mvua ikinyesha hakuna pa kujikinga. Serikali itusaidie,” akasema Bi Kamande.
Kwa upande wake, Kamishna wa Kaunti ya Lamu, Irungu Macharia alisema familia hizo zilifurushwa kwenye shamba hilo la chuo kikuu cha Egerton kufuatia amri ya mahakama iliyokuwa imetolewa awali.
“Wao wasiseme shamba ni lao. Ni dhahiri kwamba ardhi hiyo inamilikiwa kihalali na Chuo Kikuu cha Egerton. Hii ndiyo sababu tukatuma polisi kuongoza shughuli ya ubomozi na kuwafurusha maskwota hasa baada ya mahakama kutoa agizo hilo. Ninavyofahamu ni kwamba wanaojidai ni maskwota ni watu na ardhi zao na ni vyema wahamie kwenye vipande vyao vya ardhi halali badala ya kuvamia ardhi ya chuo,” akasema Bw Macharia.