Habari

Baadhi ya wanachama Knut wazidi kushinikiza Sossion ajiuzulu

August 29th, 2019 Kusoma ni dakika: 1

Na WANDERI KAMAU

BAADHI ya maafisa wa ngazi ya juu ya Chama Cha Walimu Nchini (Knut) wameingia kwa lazima katika makao makuu jijini Nairobi kwa lengo la kutaka kumng’oa uongozini Katibu Mkuu Wilson Sossion licha ya kuwepo agizo la mahakama kufuta mkutano wa Baraza Kuu la Kitaifa (Nec).

Mapema Alhamisi baadhi ya maafisa hao wamejumuika kwa madhumuni ya kumbandua katibu huyo ambaye pia ni mbunge maalumu wa chama cha ODM.

Maafisa hao kutoka maeneo mbalimbali nchini wamefika kwa mkutano licha ya mahakama kuu kuusitisha mnamo Jumatano.

Wameingia kwa lazima Knut House iliyoko katika barabara ya Mfangano Street, lakini haikubainika mapema ikiwa Sossion alikuwa ofisini wakati huo.

Vilevile wanachama wengine nao wamekita kambi nje ya makao hayo makuu.

 

Wanachama hao wanamlaumu Sossion kwa kugeuza chama hicho kuwa “mali yake binafsi”.

Wengi wao wanatoka katika maeneo ya Kati na Mashariki mwa nchi.

Wanamlaumu Sossion kwa kupendelea kanda za Nyanza na Bonde la Ufa.

Awali, maafisa wa polisi wa kupambana na ghasia walikuwa wamefika hapa lakini hakuna kisa chochote cha mifarakano ambacho kimeshuhudiwa kufikia sasa.

Bw Duncan Kanja awayewakilisha walimu kutoka eneo la Mukurwe-ini, Kaunti ya Nyeri anasema kuwa watahakikisha kuwa wamemwondoa Bw Sossion kwa kutumia njia zote hadi “uwazi na demokrasia zitakaporejea katika chama hicho.”

“Hiki ni chama cha kitaifa. Hatuwezi tukakubali kigeuzwe mali ya mtu binafsi,” amesema Bw Kanja.

Aidha, wamesema wanasubiri maamuzi ya Nec chini ya uongozi wa Bw Hezbon Ogolla.

Ni muhimu kutaja hapa kwamba kuna mkutano wa baraza hilo ambao unaendelea.