Bashir ajiuzulu, waziri afunga anga na mipaka
MASHIRIKA NA DANIEL OGETTA
RAIS wa Sudan, Hassan Umar Al-Bashir hatimaye amejiuzulu kufuatia migomo ya kila mara iliyosababishwa na bei ya mafuta kupanda.
Vikinukuu wasemaji wa jeshi, Reuters Africa na vyombo vya habari vya kiarabu Alhamisi, viliripoti kubanduliwa kwa serikali ya kiongozi huyo.
Na jioni ya Alhamisi waziri wa Ulinzi Ibn Auf alitangaza kufungwa kwa anga na mipaka ya taifa hilo.
Shirika la CNN liliripoti kuwa Bw Al-Bashir aliwekwa katika kifungo cha nyumbani huku walinzi wake wakibadilishwa.
Ripoti pia zilionyesha kuwa mazungumzo yalikuwa yakifanyika ili kutengeneza baraza la mapito.
Waziri wa Rasilimali wa Darfur Kaskazini, Adel Mahjoub Hussein kwenye mahojiano na runinga ya al-Hadath iliyoko Dubai, alisema kuwa “rais Bashir alijiuzulu.”
Asubuhi ya Alhamisi, raia wa Sudan waliandamana hadi makao makuu ya jeshi kuonyesha kughadhabishwa na uongozi wa Al-Bashir.
Kumekuwa na tetesi za mapinduzi kumwondoa rais huyu dikteta huku idhaa ya radio ya kitaifa ikiripoti kuwa jeshi linajiandia kutoa ripoti muhimu.
“Hivi karibuni, jeshi la Sudan litatoa ripoti. Twalisubiri,” akasema mtangazaji huyo bila kuongezea neno lolote.
Ripoti hizo za vyombo vya habari zilitolewa zikiambatanishwa na nyimbo za uzalendo huku waandamanaji wakifanya mkesha wa sita kwenye makao makuu ya jeshi jijini Khartoum.
Mashahidi wameambia Reuters kamba maelfu ya watu waliwasili kwenye makao hayo ya jeshi wakiimba: “ameanguka, tumeshinda.”
Magari kadhaa ya jeshi yaliingia kwenye kambi hiyo ya wanajeshi asubuhi ya Alhamisi, mashahidi waliambia AFP. Kambi hiyo pia ni makao rasmi ya Bashir na wizara ya ulinzi.
Mmoja wa waandamanaji alieleza Yousra Elbagir, mwanahabari wa Channel 4 kuwa maelfu ya watu walielekea makao ya jeshi wakionekana wenye kujawa na mbwembwe.
“Hatutaacha kuketi hapa hadi walionaswa waachwe huru na haki kutendeka kwa waliouawa.”
Alhamisi, Yousra kwenye mtandao wake wa Twitter, aliandika kuwa kuna ripoti ambazo hazijathibitishwa kwamba mmoja wa wakuu kwenye serikali ya Sudan amekamatwa na uwanja wa ndege wa Khartoum kufungwa.
Bloomberg ikinukuu idhaa ya habari ya Arabia, ikiripoti kuwa al-Bashir alikuwa na mipango ya kujiuzulu. Repoti hiyo pia ilinukuu mmoja wa walio kwenye jeshi bila kumtaja.
Kama al-Bashir atajiuzulu, atakuwa kiongozi wa pili kutoka kaskazini mwa Afrika kujiondoa mamlakani kutokana na maandamano ya taifa nzima. Rais wa Algeria Abdelaziz Bouteflika alilazimika kujiuzulu Aprili.
Al-Bashir angali anasakwa na mahakama ya ICC kwa tuhuma za mauaji ya kimbari Darfur mnamo 1989 ambako alipanda kwenye utawala kupitia mapinduzi.