BBI: Tangatanga wapanga kumzima Raila Nakuru
Na CHARLES WASONGA
WABUNGE na maseneta kutoka Rift Valley watawasilisha mapendekezo yao kwa mwenyekiti wa jopokazi la maridhiano (BBI) Yusuf Haji wala si kiongozi wa ODM Raila Odinga wakati wa mkutano wa Nakuru hapo Machi 21.
Wakiongozwa na Seneta Kipchumba Murkomen (Elgeyo Marakwet) na Seneta Susan Kihika (Nakuru), viongozi hao walisema wageni hawataruhusiwa kusimamia mkutano huo.
“Mkutano huo utaongozwa nasi kama wenyeji wa Rift Valley. Nakala yenye matakwa yetu itawasilishwa kwa Bw Haji na wanachama wake lakini sio mtu mwingine yeyote,” Bw Murkomen akasema kwenye kikao na wanahabari akiandamana na wabunge 15 kutoka Rift Valley.
Katika mikutano ya awali ya BBI katika maeneo ya Kisii, Kakamega, Kitui, Narok, Garissa, Mombasa na Meru, Bw Odinga ndiye aliyepokezwa nakala za mapendekezo kutoka kwa wakazi.
Bw Murkomen alitoa wito kwa wakazi na wageni ambao watahudhuria mkutano huo kudumisha amani akiongeza kwamba ni viongozi wachache tu ambao wataruhusiwa kuhutubu.
“Katika Rift Valley kuna zaidi ya wabunge 80 na ni wachache pekee watateuliwa kuhutubu. Vivyo hivyo, ni wageni wachache tu watapewa nafasi ya kuhutubia wananchi,” akasema.
“Nakuru ni kitovu cha amani na ndiko chimbuko la chama cha Jubilee. Kwa hivyo, hatutaki watu fulani walete siasa za matusi katika uwanja wa Afraha,” Seneta Murkomen akaonya.
“Hatutaruhusu siasa za matusi, ubabe na uchochezi ambazo zimekuwa zikiendelezwa katika mikutano ya BBI maeneo mengine,” akaongeza.
Kwa upande wake, Mbunge wa Bahati Kimani Ngunjiri alisema eneo la Rift Valley ni la kipekee kwani lina watu kutoka makabila kutoka pembe zote za nchi.
Wabunge hao walizungumza siku mbili baada ya Rais Uhuru Kenyatta kukutana na magavana kutoka eneo hilo katika Ikulu ya Nairobi kujadili maandalizi ya mkutano huo.
Rais aliitaka kamati andalizi kushirikisha viongozi wote wa Rift Valley katika mchakato huo.