Biashara haramu ya makaa inayowafaidi Al-Shabaab msituni Boni yazimwa
NA KALUME KAZUNGU
MAAFISA wa usalama katika kaunti ya Lamu wamefichua kuwa biashara haramu ya makaa na upasuaji mbao unaoendelezwa kwenye msitu wa Boni inatumika kufadhili magaidi wa Al-Shabaab.
Akizungumza wakati alipozindua operesheni kali ya kuwasaka wachomaji makaa na wapasuaji wa mbao kwenye msitu wa Boni Jumanne, Kamanda Mkuu wa Polisi wa Kaunti ya Lamu, Bw Muchangi Kioi, alisema wanabiashara wa makaa na mbao wanaoendeleza shughuli zao ndani ya msitu wa Boni wamekuwa wakiwafadhili Al-Shabaab kwa chakula na maji kupitia mapato ya biashara yao.
Bw Kioi alisema sehemu nyingi ambazo biashara ya makaa na mbao imekuwa ikiendelezwa ndani ya msitu wa Boni na vijiji vinayokaribiana na msitu huo, ikiwemo Maleli, Pandanguo na Poromoko zimekuwa zikishuhudia uvamizi wa mara kwa mara kutoka kwa Al-Shabaab.
Wakati wa operesheni hiyo, jumla ya magunia 240 ya makaa na tani kadhaa za mbao zilinaswa kwenye maeneo ya Ziwa la Kengo, Ziwa la Taa na Maisha Masha ambayo yote yanayopatikana ndani ya msitu wa Boni.
Wachomaji makaa na wapasuaji mbao wanne pia walinaswa kwenye msako huo ilhali wengine wakifaulu kukwepa mtego wa polisi.
Bw Kioi alisema maafisa wa polisi wako macho na kwamba watashirikiana na vitengo vyote vya usalama vinavyoendeleza operesheni ya Linda Boni ili kumaliza biashara ya makaa na ukataji miti kwenye misitu yote inayopatikana Lamu.
“Leo tumeamua kuzindua operesheni ya kuwasaka wachomaji makaa na wapasuaji mbao ndani ya msitu wa Boni. Tayari tumenasa magunia 240 na shehena kadhaa za mbao. Tumegundua kuwa biashara ya makaa na mbao ndani ya msitu wa Boni ndiyo inayotumiwa kuwanunulia magaidi wa Al-Shabaab chakula na maji.
Operesheni itaendelea hadi pale biashara hiyo itakapomalizwa kabisa ndani ya msitu wa Boni. Watu lazima wafahamu kwamba uchomaji makaa na ukataji mbao ni kinyume cha sheria. Marufuku ipo na lazima iheshimiwe,” akasema Bw Kioi.
Afisa huyo aidha alitoa onyo kali kwa maafisa wa usalama dhidi ya kushirikiana na wachomaji makaa na mbao katika kuendeleza biasahara hiyo kisiri.
Kwa upande wake, Afisa Msimamizi wa Shirika la Uhifadhi wa Misitu (KFS) eneo la Witu, Bw John Mbori, aliwataka wakazi, viongozi na maafisa wa usalama kushirikiana vilivyo ili kufaulisha vita dhidi ya wachomaji makaa na wakataji mbao.
“Tukiwa na ushirikiano wa dhati, ninaamini marufuku iliyopo ya ukataji mbao na uchomaji makaa itafaulu,” akasema Bw Mbori.
Operesheni hiyo imezinduliwa mwezi mmoja baada ya serikali kupitia kwa Naibu wa Rais, William Ruto, kupiga marufuku ukataji miti na uchomaji makaa kote nchini kwa siku 90 ili kuzuia athari za ukosefu wa mvua na kuhifadhi chemichemi za maji ambazo zimekuwa zikihatarishwa na kuendelezwa kwa shughuli hizo hapa nchini.